NA ABDI SULEIMAN.
WAKULIMA wa Mwani kutoka Kikundi cha Tumeamua Mtoni Msuka Magharibi, wameiyomba serikali kuwapatia boti ya kisasa itakayowafikisha kina kirefu cha maji kuweza kulima mwani ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabinchi.
Alisema kwa sasa mwani maji madogo haulimi tena, kufuatia mabadiliko hayo kwani maji yanakua moto na mwani unaungua baadhi yake kuharibika.
Wakulima hao waliyaeleza hayo kwa nyakati tofauti wakati walipokua wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, huko kwenye mashamba ya mwani Msuka Magharibi.
Asha Said Salim, mmoja ya wanachama wa kikundi hicho, alisema umaskini umepelekea kuingia katika kilimo cha mwani lakini sasa nguvu zake zinaonekana kukwama baada ya kubadilika kwa hali ya ulimaji wa mwani huo.
“Mimi siwezi hata kuogolea, leo mwani maji yenye kinakidogo haupatikani tena mpaka uwe na chombo kinachokuwezesha kufika maji makubwa huko unastawi vizuri, serikali kutuangalia na sisi kutupatia vifaa tukalima huko,”alisema.
Alisema zaidi ya miaka 30 analima kilimo hicho, fedha anazozipata huwasaidia kusomeshea watoto wake skuli na nyengine kuendeshea maisha yake.
Nae Bimkubwa Ali Bakari alisema licha ya kutokuwa na vyombo vya kufikia kina kirefu, changamoto nyengine ni ukosefu wa sehemu maalumu ya kuanikia mwani kisasa, itayoondosha tatizo la kuharibika pale unapopata Mvua au kukosa jua na kushindwa kukauka.
Alisema baada ya mwani kuongezeka bei kutoka 800 hadi kufikia 1000, kampuni za mwani zimeanza kujitokeza na kuwasaidia baadhi ya vifaa lakini sio boti za kufikia kina kirefu cha maji.
“Mabadiliko Tabianchi yametuarthiri sana sisi wakulima wa mwani, hatuna vifaa vya kufikia kina kirefu cha maji tutaweza kulima kisasa kama baadhi ya wenzetu wanavyofanya, ili kufikia huko na kupata mafanikio,”alisema.
Mkulima mwengine Binjaa Bakari Khamis, alisema mwani aliweza kulima mwani tokea kilo shilingi 300 hadi sasa 1000, huku akipendekeza kuongeza bei ya mwani hadi kufikia kilo shilingi 3000.
Aidha aliyomba serikali kuwapatia mashine ya kukaushia mwani baada ya kurudi kuvuna baharini, kwani kipindi cha mvua mwani mwingi huharibika.
Mshika fedha wa kikundi cha Tumeamua Mariyam Mikidadi Omar, alisema mwaka 2020 waliweza kuuza Tania mbili, ambapo fedha walizopata waliweza kununua vyarahani kwa ajili ya kushonea mashuka na nyengine kugawana.
Katibu wa Kikundi hicho Salama Juma Abass, alisema kikundi chao kina wanachama 25 wanachama 20 wanawake na watano wanaume, kwa sasa wanahakiba ya shilingi laki tatu benk (300,000/=).
MWISHO