Saturday, March 15

Watumishi wa umma kisiwani Pemba, wametakiwa kujenga mashirikiano ya pamoja ili kuleta ufanisi katika kazi zao.

Wito huo ulitolewa  na mkuu wa mkoa wa kusini Unguja Rashid Hadid Rashid,huko Chake Chake Kisiwani Pemba, wakati alipokuwa katika makabidhiano ya Ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Chake Chake kufuatia mabadiliko ya uongozi yaliofanyika hivi karibuni.

Rashid , aliwashukuru Masheha  kamati za ulinzi na usalama pamoja na watendaji wa Wilaya ya Cheke chake, kwa mashirikiano yao waliompa kipindi akiwa mkuu wa Wilaya hiyo, jambo ambalo limepelekea mustakabali mzuri wa utendaji wake na kumfikisha sehemu alipo.

Alimtaka mkuu wa Wilaya hiyo Abdallah Rashid Ali, kuwa karibu na watendaji wake na jamii kwa ujumla, jambo ambalo litamsaidia kupata urahisi wa kujuwa na kutatua changamoto za wananchi wa Wilaya hiyo.

” Maendeleo ya haraka hayawezi kupatikana iwapo kutakosekana mashirikiano ya kiutendaji katika Ofisi yoyote ile”,alieleza.

Nawashukuru sana masheha wangu, kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hii, bila ya kuwasahau watendaji wote wa Wilaya hii akiwemo mkurugenzi wa Baraza la mji Chake chake, kwa mashirikiano yenu mlionipa ambayo
yamenifikisha hapa nilipo.

“Nawaomba muendelee kushirikiana na mkuu wa Wilaya aliekuja, ili rikodi ya ki utendaji ndani ya Wilaya hii, iendee kufanya vizuri zaid”, alisema.

Rashid alimtaka mkuu huyo wa Wilaya ya Chake chake Abdallah Rashid Ali, kutokuwa na muhali wakati wa kufanya maamuzi, kwani kufanya hivyo kutaendana na kasi ya uwajibikaji wa Serikali ya awamu ya 8  katika
kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha  Mkuu huyo aliutaka uongozi wa Wilaya ya Chake chake kudumisha amani iliyopo, sambamba na  kuheshimu maridhiano ya kisiasa katika utoaji wa huduma kwa wananchi bila kujali itikadi ya vyama vyao, kwa kufuata taratibu za sheria, hususani katika suala la migogoro ya Ardhi na udhalilishaji.

“Jitahidi sana kufuata miongozo aliyoitoa Rais Dk, Mwinyi baada ya kuwaapisha, hususan katika suala zima la kutatua migogoro ya Ardhi kwa Wananchi pamoja na kupambana na udhalilishaji”, alisema.

Hata hivyo alimtaka mkuu wa Wilaya ya  Chakechake kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdallah Rashid Ali, alimshukuru mkuu wa Mkoa wa kusini Unguja   Rashid Hadid Rashid, kwa upendo, hekima, busara, ushauri na utendaji wake, na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo yote aliyopewa na kiongozi huyo, katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuleta maendeleo ya haraka ili dhamira ya Serikali ifikie malengo.

Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka watendaji wa Wilaya hiyo kumpa mashirikiano ya kutosha, ambayo yatajenga ufanisi wa utendaji bora.

Abdalla , alisema kuwa atahakikisha anashirikiana na Baraza la mji Chake chake, katika kuimarisha suala la usafi wa miji, kama anavyosisitiza Rais wa Zanzibar Dk, Hussein Ali Mwinyi.

Aliwashukuru wananchi wa Wilaya yake kwa kuonesha utayari wa kushirikiana nae, ingawa ni muda mchache tangu akabidhiwe wadhifa huo.

“Ni muda mchache tu tangu nishike wadhifa huu, lakini nawashukuru sana wananchi wa Wilaya hii kwa kuonesha utayari wa kunipa mashirikiano yao, na na ahidi sitowaangusha”, alisema

Mjumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ambae pia ni kamanda wa Polisi Wilaya ya Chake chake  Mohammed Mussa Mfaume, alisema mashirikiano kwao ni kawaida kwa kiongozi yoyote, hivyo alimtaka kiongozi huyo kutokuwa na muhali katika kukemea makosa pindi yakijitokeza.

Akizungumza kwa niaba ya Masheha wa Wilaya hiyo sheha wa Shehia ya Kilindi  Abuu Abrahman Salum, alisema wapo tayari kumpa mashirikiano kiongozi huyo sambamba na kupokea maagizo ya ki utendaji watakayopewa,
bila ya kuangalia umri wao.

“Tutahakikisha tutatekeleza maagizo yote tuliopata kutoka kwa mkuu wa mkoa wa kusini Unguja, ambae alikuwa mkuu wa wilaya hii na kwamba tutampa ushirikiano na huyu kiongozi mpya ambae tumepatiwa”, alieleza.

Hata hivyo Ofisa Mipango wa Wilaya ya Chake Chake   Kassim Ali Omar , aliwataka viongozi hao kumtanguliza Mwenye-enzi-Mungu mbele,  katika kila hatua ya utekelezaji wa makujumu yao.