NA HAJI NASSOR, PEMBA
MWENGE wa uhuru umewasili kisiwani Pemba, ukitokea Mkoa wa kaskazini Unguja, tayari kwa ajili ya kukimbizwa katika wilaya nne za Pemba, samba mba na ufunguzi wa miradi kadhaa, ikiwemo ya maendeleo kisiwani humo.
Mwenge huo umepokelewa jana, katika uwanja wa ndege wa Karume Pemba, ambapo wananchi wa mikoa miwili ya Pemba, wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib, wamejumuika.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahamoud, alisema mwenge huo ukiwa mkoani mwake, ulizindua miradi minane ya maendeleo na program nne, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 14.4.
Alisema wakimbiza mwenge, walitoa ujumbe kwa wananchi, ukiwemo suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira, lishe na kupinga rushwa na kisha kuchunguza afya kwa wananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa, alisema katika kipindi hichi, walipanda miti 120,000, ingawa katika shamra shamra za mwenge wamepanda miti 2,500.
‘’Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, napenda nikukabidhi mwenge wa uhuru ukiwa unang’ara, na wakimbiza mwenge wakiwa na afya njema,’’alieleza.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Abdalla Shaib Kaimu, alisema wameridhishwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo, katika mkoa wa kaskazini Unguja.
Alieleza kuwa, umoja uliopo, mshikamano na upendo ndani ya mkoa wa kaskazini, umesaidia kuwepo kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, na kuwepo kwa miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha aliwataka wakuu wa wilaya, kuwepo kwa nyaraka mahasusi ya miradi, vipimo vya kupimia ubora wa baadhi ya miradi pamoja uwepo wa wataalamu husika kwenye miradi itakayopitiwa na mwenge.
Mara baada ya kupokea mwenge huo, mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema mwenge utayapitia miradi 10 na program 10, yenye thamani ya shilingi bilioni 18.428.
Alieleza kuwa, miradi hiyo ipo katika wilaya ya Micheweni na Wete, ambapo imo ile ya maendeleo, kama ya kiwanda cha kusarifu mwani Chamanagwe, upandaji miti eneo la Kangagani.
Akisoma risala kabla ya zoezi la uzinduzi wa upandaji miti, katika kambi za chuo cha Mafunzo Kangagani eneo la Mashindeni, mpiganaji Abrahman Mwinyi Chumu, alisema ekari 792.05 zimetengwa kwa shughuli mbali mbali, ikiwemo upandaji miti.
Alisema, wameamua kupanda miti hapo, ili kulirejeshea hadhi yake eneo hilo, kufuatia uharibifu uliofanyika kwa muda mrefu, hali iliyopelekea, kuwepo kwa jangwa.
Alieleza katika eneo hilo, wanatarajia kupanda miti aina ya Mivinje 1,500 na kufanya idadai ya miti yote ambayo wataipanda hapo baadae kufikia 9,000.
‘’Katika zoezi hilo, shilingi milioni 14.175 zilikadiriwa kutumika, lakini zimeokolewa, kwa kule wapiganaji kujitolea na kutumika shilingi 13.5 kwa ununuzi wa miche,’’alieleza.
Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, alisema mikono ya wananchi, isitumike kupelekea athari kwa jamii, kwa kule kukata miti ovyo.
Alieleza kuwa, ujio wa mwenge huo katika eneo hilo, limesababisha upandaji wa miti 9000, ya aina mbali mbali ikiwemo mivinje na mikeshia.
‘’Hata baada ya kuondoka mwenge, zoezi la upandaji miti katika kambi za Chuo cha mafunzo, litakuwa endelevu, kwani tayari pameshaharibika,’’alieleza.
Mapema mkimbiza mwenge wa uhuru Zinab Hemed Mbetu, akitoa ujumbe wa mwenge, aliwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira, hasa eneo la vyanzo vya maji.
Akisoma taarifa ya kitaalamu, Mkurugenzi mkuu Kampuni ya mwani Zanzibar Massoud Mohamed Rashid, wakati mwenge huo wa uhuru ulipofika, kwenye kiwanda cha kusanifia mwani Chamanangwe, alisema ujenzi wa kiwanda hicho umefikia hatua nzuri.
Alisema ujenzi huo ambao unajengwa na Kikosi maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar ‘KMKM’ uko katika awamu ya kwanza, kati ya zile tatu hadi kukamilika kwake.
Alifafanua kuwa, awamu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa jengo kuu la kiwanda, ujenzi wa ghala pamoja na uzio maalum kwa ajili ya kulihifadhi eneo hilo.
‘’Awamu ya pili utajumuisha ujenzi wa maeneo ya bustani, ufungaji wa mitambo husika na awamu ya tatu ni kuanza uzalishaji bidhaa zitokanazo na mwani,’’alifafanua Mkurugenzi huyo.
Aidha alieleza kuwa, hadi sasa tayari ujenzi huo wa awamu ya kwanza umeshafikia asilimia 86, na ukitarajiwa kutumika shilingi bilioni 8.2 ingawa wameshatumia shilingi bilioni 4.024 na utakapomalizika wote, utagharimu shilingi bilioni 13.
‘’Mradi huu wa kiwanda, utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kusarifu mwani tani 30,000 kwa mwaka, ambapo umiliki wake kwa asilimia 55 utakuwa serikalini na asilimi 45 utakuwa wa kampuni ya Nutri-san.
Mwenge wa uhuru leo, utakuwa wilaya ya Micheweni kwa kuzindua miradi mbali mbali, kisha kukabidhiwa kwa uongozi wa wilaya ya Chake chake na Mkoani, ambapo ujumbe wa mwaka huu ‘Tunza mazingira ukoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe na uchumi wa taifa’.
Mwisho