Jamila Thabit Kombo – WHVUM
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amewasisitiza wanaharakati Vijana kushirikiana na Serikali katika kuisaidia kuielimisha jamii.
Mheshimiwa Tabia alitoa msisitizo huo wakati wa hafla ya kuwatunuku vijana Tunzo za Zanzibar Youth Award msimu wa pili, iliyofanyika katika ukumbi wa Michenzani Mall .
Amesema kupitia harakati ambazo vijana hao wanajishughulisha nazo, wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kuishawishi jamii kuondokana na matatizo mbali mbali yanayorudisha nyuma maendeleo ya Taifa ikiwemo suala la madawa ya kulevya.
Alifahamisha kuwa Zanzibar ina vijana wengi wenye uwezo, uthubutu na vipaji ambavyo vikiendelezwa na kutumika vizuri vinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo ndani ya jamii.
Aidha amewataka vijana hao kujitokeza kuwania nafasi mbali mbali katika uchaguzi wa baraza la vijana unaotarajiwa kufanyika karibuni ili kuweza kupata fursa ya kuisaidia serikali katika kutunga sera na sheria zinazowasimamia vijana.
Hata hivyo Mhe. Tabia ameahidi kutoa ushirikiano kwa Taasisi ya Zanzibar Youth Talk katika kuuwezesha mradi wa Zanzibar Youth Award kupata ufadhili wa Serikali.
Ameahidi kuwa atashirikiana na Taasisi hiyo katika kuifufua Zanzibar Music Award ili iweze kuwahamasisha vijana kukuza vipaji vyao jambo ambalo litawasaidia kupata fursa za kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Youth Talk Farida Nassor Moh’d amesema lengo la Taasisi hiyo ni kuhakikisha wanapaza sauti za vijana pamoja na kusaidia kutatuwa matatizo mbali mbali yanayowakabili.
Akisoma risala Mratibu wa Taasisi hiyo Beatrice Moshi amesema ni vyema kuziona, kuzithamini na kuziunga mkono juhudi za vijana wapenda maendeleo ambao hupambana ili kuweza kuwahamasisha kuleta mabadiliko nchini.
Zanzibar Youth Award ni Mradi ulioanzishwa na Taasisi ya Zanzibar Youth Talk mwaka 2019 kwaajili ya kuwapatia motisha vijana wanaofanya vizuri zaidi katika tasnia mbali mbali kila mwaka, ambapo kwa msimu huu wa pili wa mwaka 2020 imeweza kuwafikia vijana 3220.