NA ABDI SULEIMAN.
WAZIRI wa Maji Nishati na Madini Zanzibar Shaibu Hassan Kaduara, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), kuhakikisha kaya 90 za kijiji cha Kutukuu Wambaa Wilaya ya Mkoiani, wanawalipia huduma ya umeme ili kuondokana na tatizo la kukaa kizani.
Alisema wananchi wa kijiji hicho wamekuwa na subira ya muda mrefu kusubiri huduma ya umeme, hivyo ipo haja ya kufurahia huduma hiyo kwa kuungiwa umeme bure na ZURA.
Waziri Kaduara aliyaeleza hayo huko katika uwanja wa Mpira wa Kutukuu Wambaa, katika hafla ya kukabidhi Tansfoma kwa wananchi wa kijiji hicho kutoka ZURA.
Aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanatayarisha nyumba zao vizuri, ili kunufaika na huduma ya umeme ambayo tayari ZURA na ZECO wameifikasha.
Alisema sasa nchi ipo katika hali nzuri ya maendeleo na sasa sio kipindi cha siasa tena, chini ya miaka miwili ya Rais DK.Hussein Ali Mwinyi mambo makubwa ya maendeleo yamefanyika, ikiwemo suala la kufikishwa umeme kijijini hapo.
“Sisi nia yetu ni kuongozwa na mtu mwenye uchu wa kutuletea maendeleo, sio kuongoza na mtu ambaye haumwi na chochote kazi yake ni siasa, Dk.Mwinyi kipindi kifupi maendeleo hayo,”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanautumia umeme kikamilifu kwenye maendeleo, ikiwemo kutumia kupikia na hata biashara, ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni.
Alisema wananchi wamekua na tabia ya kuharibu mazingira kwa ukataji wa miti, kwa ajili ya kupikia, kujengea jambo ambalo linapelekea kisiwa kuwa jangwa.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Tawi la Pemba Mohamed Juma Othaman, alisema kijiji kimekaa muda mrefu bila ya kuwa na huduma ya umeme, huku Serikali ikitumia jumla ya shilingi Milioni 45 kufikisha huduma ya umeme.
Alisema fedha hizo shilingi Milioni 15.04 zimetolewa na ZURA kwa ununuzi wa Tansfoma, huku Milioni 30 zikitolewa na shirika la Umeme Zanzibar Tawi la Pemba, kwa ajili ya kukamilishia mtandao mzima wa umeme.
Meneja huyo alisema watahakikisha huduma ya umeme inafika kila maeneo hata vijijini, lengo ni kuwafanya wananchi wa kisiwa cha Pemba na Zanzibar kwa ujumla wanaondokana na tataizo la utumiaji wa Vibatari.
Akizungumzia matumizi ya umeme, aliwataka kuendelea kutunza mazingira walionayo kwa kuacha ukataji wa kuni na sasa kutumia umeme kwa kupikia.
“Sasa ni wakati wetu kutumia huma ya umeme kwa kupikia ili kupunguza uharibifu wa mazingira, ikizingatiwa sisi huko tuko visiwani na ndio waathirika wakubwa wa mazingira,” alisema.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa ZURA Zanzibar Omar Ali Yussuf, alisema kijiji cha kutukuu kilikaa muda mrefu hakina umeme, licha ya wageni kunufaika na huduma hiyo kupitia hoteli ya kitalii iliyopo.
Alisema haiwezekani kuona wazawa nawaendele kukaa kizani huku wageni wakinufaika, hali hiyo ilazimu ZURA kununua tansfoma na kuwakabidhi ZECO na kuwaungiwa wananchi huduma ya umeme.
Aliwataka wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme, pamoja na kuithamini kwani fedha zilizotumika kugharamia huduma hiyo ni fedha zao.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wananchi sheha wa shehia ya Wambaa Mohamed Suleiman, alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa kuiongoza vyema zanzibar, pamoja na kuwakumbuka wananchi wa Kutukuu.
Aidha nao wananchi wameiyomba serikali na wadau wengine wa maendeleo, kuitupia jicho la huruma barabara ya kijijini kwao kuweza kutupia jicho.
MWISHO