Friday, January 10

Skuli ya Kangagani kujengwa banda jipya la kisasa lenye vyumba vinne vya kusomea, ofisi ya mwalimu na stoo

NA ABDI SULEIMAN.

KUJENGWA kwa banda jipya la kisasa lenye vyumba vinne vya kusomea, ofisi ya mwalimu na stoo katika skuli ya Kangagani Msingi Wilaya ya Wete, litaondosha msongamano wa wanafunzi madarasani kutoka wanafunzi 120 kwa darasa moja mpaka wastani wanafunzi 45 kwa darasa.

Hayo yamebainiki kwenye zoezi la uvunjaji wa banda kongwe la vyumba vinne vya kusomea, ambalo halitumiki zaidi ya mwaka mmoja kutoka na uchakavu na ubovu la skuli hiyo lililojengwa tokea enzi za ukoloni.

Alisema ujenzi wa banda lenye vyumba hivo, unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi wa Febuari nchini ya usimamizi wa taasisi ya Nyota Foundation kupitia Mbunge wa Jimbo la Kojani.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwalimu mkuu wa skuli ya msingi Kangagani Sada Bakar Hamad, alisema kwa sasa wanalazimika kuwachanganisha wanafunzi wa madarasa mawili kwa wakati mmoja, hali ambayo mwalimu anashindwa kufundisha vizuri na kufanya ukaguzi.

“Katika mazungumzo yetu na wadau wetu hao wa maendeleo na mbunge wa jimbo hili, tumekubaliana vizuri madarasa hayo yatakuwa na fanicha zake zote, ambapo kwa sasa wanafunzi wanakaa chini, pia wanaingia mikondo miwili kutokana na wingi wao”alisema.

Aidha alifahamisha kwamba kukamilika madarasa hayo kutaondosha msongamano wa wanafunzi uliopo, huku akiitaka jamii ujenzi ukianza kutoa mashirikiano ya dhati ikiwemo suala la ulinzi wa vifaa.

Mbunge wa jimbo la Kojani ambae ndie aliyeuandiki mradi huo kwa wafadhili, Hamad Hassan Chande alisema banda linalovunjwa halikidhi mahitaji ya utowaji wa huduma ya elimu na kwamba linahatarisha usalama wa wanafunzi.

Alisema banda lililopo ni lamuda mrefu zaidi ya miaka 50, huku kukiwa kukiwa na uhaba mkubwa sana wa madarasa ya kusomea wanafunzi, kwani lengo ni kupunguza wimbi la wanafunzi na mikondo ya kuingia mara mbili.

Hata hivyo aliitaka jamii kuachana na itikadi zao katika suala la amendeleo, kwani ujenzi huo ni kwa ajili ya maendeleo ya watoto wao.

Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya maandalizi na msingi Kombo Khamis Bakar, alishukuru wananchi kwa kuondosha tafauti zao katika ujenzi huo, kwani wameona kinachofanywa ni kwa ajili ya watoto wao.

“Jenge lililokuwepo sio kongwe bali ni bovu na lilikuwa hatarishi kwa maisha ya wanafunzi, lilihamwa zaidi ya mwaka mmoja, huku tukiwa tumesha hangaika sehemu mbali mbali na sasa tumefanikiwa kupitia Mbunge wa Jimbo la Kojani kutafuta mfadhili ndio tumo katika maandalizi kuvunja na tuanze ujenzi”alisema.

Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi ya skuli hiyo Mbarouk Hamad Yussuf, alisema kuvunjwa kwa jengo hilo na kujengwa jipya kutasaidia kwanza kupata nafasi ya watoto kusoma katika mazingira mazuri, hata mazingira ya ufundishaji yatakuwa mazuri.

Aidha alisema pia jengo hilo litasaidia kukuza vipaji vya wanafunzi na kufanya vizuri katika mitihani yao ya taifa na kufikia ndoto walizojiwekea.

Ujenzi wa jingo jipya la kisasa la skuli ya msingi Kangagani litajumuisha uwekaji wa fanicha ambapo 70% zitatolewa na mfadhili na 30% ni za wananchi.