NA ABDI SULEIMAN.
MWENGE wa Uhuru kitaifa 2023 umewasili Mkoani Tanga, baada ya kumaliza mbio zake Mkoa wa Kusini Pemba, ambao umekimbizwa kilomita 138.9 na kuweka jiwe la msingi, kuzindua na kukagua miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 2,135,899,033.10.
Akisoma risala ya makabidhiano ya Mwenge huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, Katibu Tawala Mkoa huo Amour Hamad Saleh, alisema kati ya fedha hizo shilingi Bilioni 1,117,130,601 sawa na asilimia 52.3 kutoka serikali kuu, shilingi 117,923,334 sawa na asilimia 5.5 ni michango ya wananchi na shilingi 900,845,097.73 sawa na asilimia 42.2 michango kutoka kwa wahisani.
Alisema kati ya miradi hiyio, miradi sita iliwekewa mawe ya msingi, mmoja ulizinduliwa na miradi minne ilikaguliwa na mmoja ulifunguliwa.
Akizungumzia hali ya usalama ndani ya Mkoa huo, alisema kwa sasa ni shwari na salama, kwani wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi, kijamii, utulivu na mashirikiano makubwa.
Kwa upande wa suala la Mapambano ya Mamlaka ya kuzuwia rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), kipindi cha Julai 2022-Madi 2023 Jumla ya matukio 45 yameripotia, ambapo majalada sita yapo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua za kisheria, 27 yapo katika hatua mbali mbali za uchunguzi, sita yamefutwa na sita yamehamishiwa taasisi nyengine kwa kua matukio hayo hayakua na mnasaba wa rushwa.
Kuhusu suala la Dawa za Kulevya, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 jumla ya matukio 36 yameripotiwa, kati ya hayo 20 ni bangi, 14 ni heroin, moja ni Valium na moja Codeine, huku matuko 20 yapo mahakamani na saba yameshatolewa hukumu na tisa yapo katika hatua za upelelezi.
Katika mapambano dhidi ya Malaria nchini ya kauli mbiu nipo tayari kutokomeza Malaria, Wewe Je?, kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, jumla ya vyandarua 25,011 viligawiwa kwa wananchi 13,839 Wilaya ya Chake Chake na 11,172 Wilaya ya Mkoani.
Hata hivyo katibu huyo alisema katika kupambana na janga la VVU chini ya Kauli Mbio “Pima, Jitambue, Ishi”Jumla yay a wananchi 13,567 walipatiwa ushauri nasaha wanaume 7,021 na wanawake 6,546.
Naye katibu Tawala Mkoa wa Tanga Pili Hassan Mnyema, alikiri kuupokea mwege huo baada ya kutoka Mkoa wa Kusini Pemba, alisema mwenge huo utakimbizwa katika halmashauri 11 na umbali wa kilomita 1959 na kufanyia kazi Miradi 92 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 27
MWISHO