Monday, November 25

DK.HUSSEIN MWINYI AZUNGUMZA NA TAASISI YA ULINGO NA KUKABIDHIWA TUZO MAALUM

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Tanzania inatambua na kuheshimu usawa wa kijinsia kwa kuona umuhimu wa kuwachagua wanawake kwenye mihimili yote ya Serikali, Bunge na Mahakama kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo, Ikulu, Zanzibar alipozungumza na uongozi wa taasisi ya kiraia, inayounganisha Jumuiya za wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa vyenye usajili kamili nchini, tasisi ya Sauti ya wanawake wenye ulemavu (SWAUTA), Chama cha wabunge wanawake (TWPG) na Umoja wa wanawake wa Baraza la Wawakili (UWAWAZA). T-WCP – ULINGO. Waliofika kumkabidhi tunzo ya hongera kwa mafaniko makubwa aliyofanya ndani ya muda mfupi wa uongozi wake.
Alisema, Serikali zote mbili zitaendelea kutoa fursa za kutosha kwa wanawake kwenye maeneo mbalimbali ili kutekeleza azma yao kufikia 50 kwa 50.
Alisema, maendeleo yana taka usawa wakijinsia ili kutoa haki na fursa sawa katika maendeleo ikiwemo elimu, afya na jamii kwani kumuelemisha mwanamke kutaondoa changamoto nyingi kwenye jamii.
“Sijajuta hata kidogo kwa wale wanawake niliowateua kwenye Serikali yangu, kwa kweli naona umuhimu wa kuwaongeza kwenye safu mbalimbali” Alibainisha Rais Dk. Mwinyi.
Alisema, Serikali pia itaendelea kuimarisha huduma za mama na mtoto ili kupunguza changamoto nyingi kwa wanawake.
Rais Dk. Mwinyi pia, aliwapongeza ULINGO kwa kazi kubwa wanayoifanya kuunganisha pamoja sauti ya pamoja, na kuwasifu hatua yao ya kutanguliza maslahi mapana ya taifa kwa kuunganisha nguvu ya umoja wao bila kujali tofauti ya itikadi zao za kisiasa pamoja na kuwashirikisha wanawake wengi na kuwashajihisha kitaaluma kujua haki na wajibu wao kwenye masuala ya haki na siasa.
Alisema, katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa haki kwa jinsia zote kushiriki katika masuala  ya siasa. Pia Dk. Mwinyi aliahidi kuipokea tunzo hiyo kama sehemu ya kuongeza za kuweka fursa sawa za jinsia kwenye maeneo yote.
Nao, viongozi wa taasisi hiyo wamempongeza Dk. Mwinyi kwa kutekeleza kwa vitendo masuala ya usawa wa kijinsia na ujumuishi wa makundi maalum katika ngazi mablimbali za maamuzi, kulinda na kudumisha amani, umoja na utulivu nchini na kushajihisha umoja wa kitaifa pamoja na masuala ya msingi kwa maendeleo endelevu.
Pia, walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kutambua kikwazo kikubwa kinachowanyima fursa wanawake ikiwemo ukosefu wa elimu, changamoto kwenye sekta ya afya kwa kuweka miundombinu imara ili kukabiliana na changamoto pamoja na huzitatua kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.
Akizungumza kwenye halfa hiyo kwa niaba ta Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Anna Magareth Abdalla, Makamo Mwenyekti wa taasisi hiyo kwa Zanzibar ambae pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan alimuahidi Dk. Mwinyi mwaka 2025 atarejeshwa tena madarakani kwa nguvu na umoja wa wanawake nchini ambao kwasasa sauti yao ni moja tu ya kudumisha amani ya nchi na maendeleo kwa maslahi mapana ya taifa.
Pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Mwinyi kwa kwa mageuzi makubwa aliyoiletea Zanzibar kupitia sekta za Afya, Elimu na Uchumi wa Buluu pamoja na kuongeza fursa za uongozi na maendeleo kwa wanawake na kumuahidi daima wanamuunga mkono katika kuiletea maendeleo makubwa Zanzibar.
Wakati huo huo, viongozi hao walifika Ofisi za taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF)” Migombani na kuzungumza na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi walimpongeza kwa jinsi anavyojitoa na kuwapigania wanawake, vijana na watoto kimaendelea, ikiwemo kuwainua kiuchumi, elimu na afya pamoja na kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mama Mariam Mwinyi alieleza ULINGO na taasisi yake ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF)” zinapaza sauti moja na dhamira sawa za kumkomboa mwanamke kutambua haki zake ili aondokane na mazila ya ugumu wa maisha kwa kuzikimbilia fursa za maendeleo na kuzitambua haki zao za msingi.
Alisema ZMBF ni chachu ya maendeleo ya wanawake, vijana na watoto dhidi ya changamoto wanazokumbana  nazo kwenye jamii, zikiwemo za afya, elimu na jamii kwa kushajihisha wanawake kuinuka kiuchumi kupitia ukulima wa mwani, kupinga udhalilishaji wa watoto, kusaidia wanawake kuzingatia lishe bora ili kuimarisha afya za mama wajawazito na kuepusha vifo wakati wa kujifungua, kushajihisha jamii kufanya mazoezi ili kujizuia na maradhi yasiyoambukiza yakiwemo moyo, kisukari na saratani pamoja na kumsitiri mtoto wa kike aendelee kuwa kwenye hedhi salama kwa mustakbali mzima wa maendeleo yake kielimu.
IDARA YA MAWASILIANO – IKULU, ZANZIBAR