Majina ya wateule wa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2022, yanatarajiwa kujulikana Juni 23, 2023 katika kikao kati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na waandishi wa habari kitakachofanyika katika ukumbi wa hotel ya The Diplomat ya jijini Arusha.
Katika mashindano hayo, jumla ya kazi 893 ziliwasilishwa kutoka vyombo vya habari vya magazeti, radio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni.
Jopo la majaji saba, wenye utaalamu katika habari radio, runinga, magazeti na vyombo vya habari vya mtandaoni walifanya kazi kwa siku tisa ili kupitia kazi hizo.
Majaji hao wakiwa chini ya Mwenyekiti, Mkumbwa Ally walifanya kazi hiyo kuanzia Juni 10 mara baada ya kuapishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Robert Makaramba Juni 9, 2023.
Jopo hilo lilikuwa na wajumbe wafuatao Rose Haji Mwalimu, Mbaraka Islam, Peter Nyanje, Nasima Chum, Dk. Egbert Mkoko na Mwanzo Millinga aliyekuwa Katibu wa jopo hilo.
Washindi waTuzo hizo watatangazwa katika kilele cha mashindano hayo Julai 22, 2023 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Hii itakuwa ni mara ya 14 mfululizo tuzo hizo zinafanyika hapa nchini. Tuzo hizo zilianza kufanyika mwaka 2009, na zimeendelea bila kukosa hata mara moja.
Katika kilele cha mwaka huu, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tuzo hizo, zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Julai 22, 2023, katika ukumbi wa Mlimani City. Jaji Chande ni Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Haki Jinai.
Mwisho.
(CHANZO CHA HABARI MCT)