Mamlaka zinzosimamia huduma za usafirishaji kwa njia ya maji zimetakiwa kuzingatia na kusimamia vyema maslahi ya mabaharia wanapokua kazini.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Masoud Makame ametoa agizo hilo akimuwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakati akifungua rasmi maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani yaliofanyika katika viwanja vya furahisha jijini Mwanza.
Mhe. Suleiman Makame amesema kuwa, mabaharia wanafanya kazi kubwa sana katika kutoa huduma za usafirishaji wa binadamu na bidhaa mbali mbali kwa njia ya maji.
Aidha, Mhe. Waziri ameeleza kwamba sekta ya ubaharia imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuinua pato la taifa na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Amesema Serikali zote mbili kupitia viongozi wake zimekuwa zikichukua jitihada za maksudi ya kutoa msukomo katika kukuza uchumi wa buluu ambapo kwa upande wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imenunua meli kadhaa pamoja na kujenga meli mpya itakayohudumia katika eneo la kanda ya ziwa.
Pia, kwa upande wa Zanzibar ameeleza kwamba Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akichukua jitihada kubwa za kuwawezesha wananchi wake kushiriki kikamilifu kwa kuinua kipato chao kupitia dhana ya uchumi wa buluu.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Suleiman Makame amewataka wananchi kuacha kabisa tabia ya kuharibu mazingira kwa kutupa au kutirirsha takataka zenye sumu ndani maji ili kuepusha uharibifu wa viumbe hai.
Kupitia maadhimisho hayo yaliofanyika jijini Mwanza Mhe. Waziri amewataka washiriki wa maadhimisho hayo kuelezea kwa kina faida zitokanazo na fursa zinazopatikana katika maji kwani kufanya hivyo, itakuwa wameitendea haki siku hiyo adhimu kwa mabaharia Duniani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar (ZMA) Ndugu Sheikha Ahmed Mohamedamesema Tanzania inaungana na mataifa yote duniani kudhimisha siku hiyo ikiwa na kauli mbiu “miaka 50 ya Marpol uwajibikaji wetu unaendelea”
Katika kuhakikisha Tanzania inaekwenda sambamba na Ulimwengu Tanzania imeridhia mikataba ishirini na mbili (22) ya kimataifa ilioridhiwa na shirika la bahari Duniani (IMO).
Mkurugenzi Mkuu Sheikha Ahmed ametoa wito wa kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Srikali na taasisi mbali mbali katika kulinda mazingira ya baharini pamoja mito na maziwa.
Akisoma risala kwa niaba ya jumuiya za mabaharia Katibu Ndugu Ali Mzee Ally amesema yapo mafanikio kadhaa yaliofikiwa kupitia sekta hiyo ikiwemo kupatika kwa mabaharia wasiopungua Elfu moja (1,000) waliofunzwa vyema na kufanya kazi ndani na nje ya nchi sambamba na ajira za meli za uvuvi zimeanza kupitia katika vyama vya mabaharia.
Pia, Katibu huyo ametoa mapendekezo kwa Serikali kwa kuomba kuwepo kwa miongozo yenye kujumuisha haki na ulinzi katika sehemu za kazi, kuhakikisha ushindani kibiashara wenye kuzingatia haki.
Mapema, Mhe. Waziri alitembelea na kukagua maonesho yalioandaliwa katika maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (WUMU)