Friday, January 10

WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kushirikiana pamoja na Mradi wa viungo Zanzibar katika kuhakikisha wanaelimisha wakulima wa viungo kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 

WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kushirikiana pamoja na Mradi wa viungo Zanzibar katika kuhakikisha wanaelimisha wakulima wa viungo kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora, ili ziweze kukidhi vigezo katika soko la ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi hao katika Ukumbi wa Ofisi ya Chama Cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi huo, Ali Abdalla Mbarouk alisema, wakulima wanatakiwa kuongeza thamani na wingi wa bidhaa kwa kutumia mbinu za kisasa.

Alisema kuwa, ipo haja elimu itolewe kwa wakulima wa viungo ili kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora, hali ambayo itakubalika na kuwa na uhakika wa soko, kwani wakati mwengine wanatokezea mataifa ya nje kutaka bidhaa, ingawa hukosa kutokana na kiwango kinachozalishwa kuwa ni kidogo.

“Bidhaa za kwetu zinakubalika sana kimataifa, lakini zaidi huhitaji kwa tani na sio kwa kilo, jambo ambalo linatukwamishwa kwani hatuzalishi kwa wingi, hivyo waandishi tushirikiane kutoa elimu ili wakulima waelewe hili”, alisema Afisa huyo.

Alieleza kuwa, katika kuhakikisha wakulima hao wanazalisha kwa wingi na kupata soko, watashirikiana na wadau mbali mbali wanaohusika, ili kuleta uchumi shirikishi utakaosaidia kuwaongezea kipato.

“Lengo kuu la mradi ni kuongeza uzalishaji kwa kufuata mabadiliko ya tabianchi, kuwafundisha wakulima mbinu bora za kilimo na kusaidiwa pembejeo, kuwepo uhakika wanchakula, kuongeza thamani na masoko pamoja na kuongeza kipato kwa wakulima”, alifafanua.

Kwa upande wake afisa Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kutoka mradi huo, Asha Mussa Omar alisema, waandishi wa habari wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko kwa wakulima hao, hivyo watumie vyombo vyao vya habari kuelimisha kuona kwamba uzalishaji unaongezeka zaidi ili, watakapokuja wateja bidhaa zipatikane kwa wingi.

Alisema kuwa, wanataka waboreshe hali za wakulima hususan wanawake ambao imeonekana ni kundi lililoachwa nyuma kwa muda mrefu.

“Mradi wetu utashughulika na wakulima wa viungo, mboga na matunda, hivyo tutahakikisha tunaongeza thamani ya bidhaa zao, soko, lishe pamoja na kuwaongezea eneo la uzalishaji”, alieleza.

Nae Afisa Biashara wa mradi huo Omar Mtarika Mselem alisema, mradi huo utahakikisha wakulima wanalima kulingana na soko hali ambayo itasaidia kuboresha soko na kuwepo kwa uhakika wa bidhaa zinazozalishwa.

“Katika miradi iliyopita tumekuwa tukiwatafutia wakulima masoko katika mahoteli lakini tunashindwa kutokana na masharti ya kuwa bidhaa wazipate muda wote sio kwa msimu, jambo ambalo wakulima wetu hawana, hivyo kwa  sasa tunataka tuachane na ukulima wa msimu, huu ni wakati wa kulima kila siku”, alifahamisha.

Kwa upande wao waandishi wa habari walisema kuwa, ni jambo zuri watakalolifanya mradi huo, kwani wanaamini wakulima wengi watapata kipato kitakachowakwamua kiuchumi.

“Ombi letu ni kuona kwamba utakapomaliza mradi huu ionekane mabadiliko ya wakulima, waweze kuendesha maisha yao ya kila siku kupitia kilimo chao, kwa sababu tumeshuhudia miradi mingi inapomaliza haiendelei na hali za wakulima hazibadiliki”, walisema waandishi hao.

Mradi huo wa viungo Zanzibar unaotekelezwa na TAMWA, Jumuiya ya kuhifadhi misitu asili Pemba (CFP) na Shirika la PDF la Dar-es-Saalaam, ambao unasimamiwa na Serikali chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.