Thursday, November 14

Huduma ya nishati ya  umeme yabadilisha Kisiwa cha Njau.

NA SAID ABRAHAMAN-PEMBA

WANANCHI wa Kisiwa Cha Njau Wilaya ya Wete wamesema kuwa kupatikana Kwa huduma ya nishati ya  umeme katika Kisiwa Chao kumeweza kubadilisha maisha yao.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi wananchi hao walisema kuwa kabla ya kuwepo Kwa nishati ya umeme ndani ya Kisiwa hicho ilikuwa ni shida kubwa kwao.
Bakari Khamis Hamad Mkaazi wa Njau (mvuvi) alieleza kuwa kabla ya kufika nishati ya umeme ndani ya Kisiwa Cha Njau changamoto kubwa waliyokuwa nayo ni kuuza Kwa bidhaa zao (samaki, pweza) Kwa hasara kutokana na kushindwa kuwahifadhi   jambo lilikuwa likiwarudisha nyuma kimaendeleo.
“Muda huo ilitupasa tufanye hivyo kutokana na ilikuwa hatuna njia nyengine yeyote ile ya kuweza kuhifadhi bidhaa zetu Kwa haraka haraka,” alisema Bakar.
Hata hivyo Bakar alisema kuwa baada ya kufika nishati hiyo ndani ya Kisiwa Chao mambo mengi yamekuwa yakienda sawa na Kwa Sasa kila kile ambacho wanakivua Wana uwezo wa kukihifadhi katika mafriji na kuuza Siku ya pili yake.
“Tunaishukuru Serikali yetu ya Mapinduzi ya Zanzibar Kwa kutuletea huduma ya umeme katika Kisiwa chetu kwani hivi Sasa tuna uwezo wa kuhifadhi pweza Hadi kufikia kilo 100 na hapo huwatoa na kutafuta soko ambalo litakidhi haja,” alisema Bakar.
Sambamba na hayo Bakar alifahamisha kuwa hapo zamani iliwalazimu kupeleka simu zao katika Kijiji Cha Gando Kwa ajili ya kuwekewa chaji jambo ambalo kwao lilikuwa ni usumbufu Mkubwa kwani muda mwengine hutokezea simu hizo kuingia katika bahari au kuroa Kwa mvua wakati wakivuuka.
Kwa upande wa miundombinu ya nishati hiyo, Bakar alieleza kuwa Hadi sasa hakuna hitilafu yeyote kubwa ambayo imejitokeza ambayo imewakosesha huduma  bali ni changamoto za kawaida na hivyo huweza kusaidiana na wataalamu wa Shirika la Umeme Ili kuweza kulitatua.
“Kwa Sasa hakuna changamoto kubwa ambayo imejitokeza, lakini pia umeme wa jua ni nzuri tu, Mimi naweza kusema kuwa umeme huu hauna tofauti ule wa kawaida,” alieleza Bakar.
“Licha ya changamoto zinatokezea lakini bado Kuna mashirikiano makubwa baina ya mafundi wa Shirika la Umeme kwani wako vizuri katika kuhakikisha huduma hii inawafikia ipasavyo,” alisema Bakar.
Nae Juma Ali Mkaazi wa Njau Wilaya ya Wete alieleza kuwa tokea kupatikana Kwa huduma ya umeme katika Kisiwa Cha Njau, matatizo mengi yamepungua kwani  kabla ya hapo walikuwa wakipata usumbufu.
Juma alisema kuwa baada ya kufika Kwa mradi huu wa umeme maendeleo makubwa yamepatikana Kwa wakaazi wote wa Njau Kwa wale ambao Wana mafriji na hata wasio na mafriji.
“Hivi Sasa tumeanza kusahau matumizi ya vibatali kwani ukiangalia asilimia kubwa ya wananchi wake tayari wameshaungiwa umeme na Bado wachache ila tunaimani kuwa nao watapata huduma hii muda mfupi tu,” alieleza Juma.
“Nikuzungumzia kipato changu Kwa Sasa, namshukuru sana Mwenyezimungu mambo ni mazuri ukilinganisha na hapo nyuma tulipotoka hivi Sasa Kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi”, alifahamisha Juma.
Juma akitoa wito Kwa Serikali kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha Kisiwa Cha Njau kinapata huduma ya maji safi na salama bila ya usumbufu wowote ule.
              MWISHO