Thursday, November 14

Soko la mboga mboga na matunda Tondooni Pujini kujengwa la kisasa.

NA ABDI SULEIMAN.

MWAKILISHI wa Jimbo la Chonga Wilaya ya Chake Chake Suleiman Massoud Makame, amesema kuwa suala la maendeleo kwenye serikali ya awamu ya nane hayana chama ni kwa ajili ya wananchi wote wa Zanzibar.

Alisema wanachama wa CCM, ACT Wazalendo, CUF na vyama vyengine wote wananufaika na maendeleo yanayoletwa nchini, ikiwemo barabara, hospitali, skuli, maji safi na salama, umeme na masoko.

Mwakilishi huyo aliyaeleza hayo, wakati akikagua maendeleo yaliyofikiwa ya soko la mboga mboga na matunda Tondooni Pujini jimbo la Chonga Wilaya ya Chake Chake, wakati waziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo jimboni humo.

Alisema bado dhamira yake iko pale pale ya kuhakikisha soko hilo, linamalizika kwa wakati na wananchi wanafanya biashara zao mbali mbali ndani.

“Niliwahidi wananchi na wazee wangu nakumbuka hapa palikua na kibanda cha makuti, nikasema wapo walioamini na wasioamini leo lipo hili, nitahakikisha linakua la kisasa hili na kila mtu anafanyabiashara zake,”alisema.

Aidha alisema Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi anahimiza suala zima la maendeloe kwa wananchi wake, hivyo wawakilishi wamekuwa wakimuunga mkono Rais kwenye kupeleka maendeleo hayo kwa wananchi wake.

Katibu wa CCM jimbo la Chonga Yussuf Hamadi Kombo, alisema ujenzi wa masoko ya kisasa, skuli za gorofa, barabara kiwango cha lami hadi vijijini vyote vinatokana na uongozi wa serikali zote mbili.

Alisema viongozi wa nchi SMT na SMZ wamekuwa wakihangaika kuhakikisha wananchi wa Tanzania, wanaishi katika maisha bora na kupatiwa huduma zote muhimu bila ya kujali itikadi ya chama Fulani.

“Uwepo wa soko hili ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya uchaguzi, lakini halitokua la wanachama Fulani bali ni lawananchi wote wa tondooni,”alisema.

Aidha aliwataka kuthamini juhudi za maendeleo zinazifikishwa na viongozi wao, kwa kuhakikisha wanafanyia kwa kuondosha tafauti zao na kuwa kitu kimoja kwenye maendeleo.

Nae kada wa CCM jimbo la Chonga Heri Juma Basha, alisisitiza suala la umoja mshikamano ndani ya jamii, ili kuleta faraja ndani yao na nchi kwa ujumla.

Alisema wananchi wanapaswa kujadili juu ya changamato zilizopo ndani ya jimbo lao, watazitatua vipi na sio kuwepo kwa mambo mengine ambayo hayako katika maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Juma Khamis mkazi wa Tondooni Pujini, alisema kilio kikubwa chao ni mwendo kasi wa maedereva wa gari  za mizigo, abiria na piki piki wanaopita katika kijiji chao, hivyo wanaomba kuwekewa matuta katika barabara hiyo ili kupunguza ajali.

Alisema zaidi ya ajali 10 tayari zilishatokea katika kijiji cha Tondooni, huku wakisikitishwa na kutokunufaika na fursa za rasilimali zisizorejesheka zinazotoka katika kijiji chao.

MWISHO