Monday, November 25

KIJALUBA iSAVE yawafundisha walimu mbinu usimamizi vikundi vya wenye Ulemavu

JUMLA ya Viongozi 86,  Unguja 40 na Pemba 46 wa vikundi vya kuweka na kukopa kupitia mradi wa KIJALUBA iSAVE wamepatiwa mafunzo maalum ya usimamizi wa uchukuaji mikopo na sheria za vikundi ili kuimarisha ustawi wa uchumi wa wanachama kwenye vikundi vya watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo ambayo ni utekelezaji mradi wa KIJALUBA iSAVE ZANZIBAR unaotekelezwa kwa mashirikiano ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania,Zanzibar (TAMWA-ZNZ), na Shirikisho la Jumuiya za  Watu wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) kupitia ufadhili wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu ya Norway (NAD) yamekuja kufuatia zoezi la uundaji wa vikundi ambavyo vinawashirikisha watu wenye ulemavu kukamilika na kuanza kutoa mikopo kwa wanachama.
Katika mafunzo hayo viongozi wamefundishwa pia misingi bora ya kuweka kumbukumbu katika vikundi vyao ili kuepusha migogoro inayotokana na upotevu wa taarifa muhimu za wanachama kwenye kikundi.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Pemba Bakari Haji alisema mafunzo hayo yatakwenda kusaidia wahusika kutekeleza majukumu yao na kuongeza kasi ya ufikiaji mafanikio ya watu wenye ulemavu katika vikundi vyao na kuondokana na utegemezi kiuchumi.
Nae mwezeshaji kutoka Unguja Muhidini Ramadhan aliwashauri viongozi wa vikundi kusimamia na kuyatumia mafunzo hayo waliopewa ili waweze kuendesha vikundi kwa mujibu wa muongozo wa mradi ili kukuza uchumi jumuishi kwa watu wenye ulemavu katika jamii.
Wakizungumza wakati wa mafunzo hayo walimu wa vikundi wamesema mafunzo yatawasaidia kutekeleza majukumu yao na kuvisimamia vikundi hivyo kwa kutoa mwongozo wa uendeshaji vikundi hasa kwa wenye ulemavu ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Mohamed Ali, msimamizi na mwalimu wa vikundi Unguja alishukuru kutolewa kwa mafunzo hayo kwani licha ya kuwa na uzoefu katika usimamizi wa vikundi lakini ameongeza ujuzi zaidi wa namna ya kusimamia vikundi vya watu wenye ulemavu kutokana na kuhitaji usimamizi maalum.
Alieleza watu wenye ulemavu wanahitaji kupatiwa mbinu na usimamizi rafiki ili kuhakikisha rasilimali za vikundi hazipotei na badala yake kuleta manufaa kwao kujikomboa kiuchumi jambo ambalo litatekelezwa kupitia ujuzi walioupata.
Nao viongozi wa vikundi hivyo wameshukuru kupatiwa mafunzo hayo na kuahidi kwenda kuyatumia vyema na kuyafikisha kwa wanakikundi wenzao ili waweze kiuendesha vikundi kwa mujibu wa muongozo na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Mradi wa KIJALUBA ni mradi jumuishi unaolenga kuwakomboa kiuchumi watu wenye ulemavu ambao unatekelezwa kwa majaribio ndani ya wilaya mbili za Zanzibar, kwa Unguja wilaya ya Kusini na wilaya ya Chake chake Pemba ambapo tayari umeunda jumla ya vikundi 43.