Sunday, November 24

Wakala yajidhatiti kuwainua wananchi kiuchumi.

 

KAIMU Mratibu wa wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar Ofisi ya Pemba Haji Mohamed Haji, akiwasilisha taarifa ya miradi inayotekelezwa na wakala mwaka 2023/2024, huko katika ukumbi wa Wizara hiyo Gombani.
BAADHI ya wakuu wa maidara kutoka Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Pemba, wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa taarifa ya miradi inayotekelezwa na wakala wa uwezeshaji 2023/2024, huko katika ukumbi wa Wizara hiyo Gombani
MENEJA kutoka Idara ya Huduma za Jamii Ofisi ya Rais Ikulu, Dr.Ibrahim Kabole akizungumza katika kikao cha kuimarisha ufanisi wa kiutendaji na kuhakikisha Rasilimali zonatumika kwa ufanisi, kikao kilicho washirikisha watendaji kutoka Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais kazi uchumi na uwekezaji Pemba, na kufanyika Gombani

.(PICHA NA ABDI SUELIMAN, PEMBA)

NA ABDI SULEIMAN.

WAKALA wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar, imesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 inakusudia kutekeleza programa mbali mbali, ambazo zimelenga kuwainua wananchi kiuchumi kupitia miradi ya uzalishaji.

Aidha program ambazo zimekusudiwa kutekelezwa na wakala huyo ni pamoja na Programu ya Mikopo Inuka (COVID-19), programu ya Halifa Fund, programu ya 4.4.2, programu ya Mfuko wa Uwezeshaji na programu ya Mfuko wa Mboga Mboga na Matunda.

Hayo yalielezwa na kaimu Mratibu wa wakala wa Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar Ofisi ya Pemba Haji Mohamed Haji, wakati akiwasilisha taarifa ya miradi hiyo, wakati wa kikao cha kuimarisha ufanisi wa kiutendaji kwa taasisi zinzotekeleza miradi hiyo huko Gombani.

Alisema programu hizi zote, zimelenga kuwainua wananchi kiuchumi kupitia Miradi ya Uzalishaji katika sekta kilimo, ufugaji, uvuvi, ushoni, ufinyanzi, viwanda vidogo vidogo na vya kati, useremala, ukulima wa mwani na mama lishe.

Alifahamisha kwamba wakala wa Uwezeshaji itaendelea kutekeleza mradi wa utoaji wa Vifaa vya Nyuki na kuendeleza kituo cha kuchakatia mazao ya Asali Pujini Pemba.

Kaimu Mratibu huyo alisema program ya Inuka (COVID-19), ilianza March 2022 na ipo katika utekelezaji na imeingia katika utekelezaji wa mwaka wa Fedha 2023/24, ikiratibiwa na ZEEA kwa kushirikiana na Bank ya CRDB, kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasirimali na wafanyabiashara wote wa Zanzibar.

Alisema tageti ya programu hii ni kuwafikia wanufaika 62,400 Unguja na Pemba kwa muda wa miaka 5 sawa na wanufaika 12,480 kwa mwaka (20%).

Aidha hadi kufukia June 2023 zaidi ya shilingi 7,484,912,684.20 zimeshatolewa kwa wanufaika wanaume 3785 na wanawake 5691 kwa Wilaya nne za Pemba ikiwemo Micheweni, Wete, Chake Chake na Mkoani.

Kwa upande wa program ya mfuko wa mboga mboga na matunda, ilianza kutoa huduma ya Mikopo kwa wananchi mwaka 2018, na imelenga kuwainua Wakulima wa Mboga Mboga na Matunda pamoja na kuongeza samani ya Mazao Unguja na Pemba.

Alisema mpaka kufikia June 2022 Mradi huu umeweza kufikia walengwa 601 katika sekta ya kilimo cha mboga mboga na matunda kutoka kutoka Wilaya nne za Pemba na zaidi ya shilingi 444,900,000 wameshapatiwa

kwenye program ya mfuko wa Uwezeshaji ilianza mwaka 2003, na imejikita katika kuwainua wajasirimali na wafanya biashara katika sekta mbali mbali, mpaka kufikia June 2022 jumla ya wanufaika 1374 kwa upande wa Pemba na zaidi ya shilingi Milioni 893, 257,000.

Akizungumzia changamoto za wakala alisema ni kutokuwepo kwa kituo cha kukuza na kulea, uhaba wa rasilimali watu na vifaa, kutokuwepo kwa Mifumo madhubuti ya kuendeshea, kusimamia na kihifadhi taarifa za mikopo na dhana potofu kwa Baaadhi ya wakopaji.

Mapema meneja Idara ya huduma za jamii Ofisi ya Rais Ikulu, Dr.Ibrahim Kabole, alivitaka vitengo vinavyosaidia vijana na wajasiriamali kukaa sehemu moja ili wajasiriamali waweze kunufaika na maendeleo ya serikali ya awamu ya nane.

MWISHO