Friday, January 10

Akina mama washauriwa kuacha kula vyakula visivyostahiki wakati wa ujauzito.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

AKINAMAMA wajawazito wametakiwa kuacha tabia ya kula vyakula visivyostahiki kwani inawasababishia upungufu wa damu mwilini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa TAMWA Mkanjuni Chake Chake katika mafunzo ya Afya ya uzazi, Dk. Rahila Salim Omar alisema kuwa, kuna baadhi ya akinamama wajawazito wana tabia ya kula mchele, udongo, mkaa na vitu vyengine visivyostahiki, jambo ambalo sio sahihi.

Alisema, ni vyema kwa akinamama hao kuacha mara moja kula vyakula visivyostahiki, ili kuepuka upungufu wa damu pamoja na kumsaidia mtoto kumuepusha na madhara yanayoweza kumpata.

“Wajawazito wengi wanakula vitu ambavyo sio sahihi kwa afya, hii husababisha kupungukiwa na damu na wakati mwengine madhara yanampata mtoto”, alisema daktari huyo.

Aidha Dk. Rahila aliwashukuru akina mama hao kula vyakula vyenye lishe ili awe salama yeye na mtoto wake, tangu siku ya kutunga mimba mpaka kumlea mtoto.

“Akinababa msikimbie majukumu yenu, muhakikishe munawahudumia vizuri wenza wenu hasa pale wanapokuwa wajawazito, hii itasaidia kuimarika kiafya pamoja na mtoto atakaezaliwa”, alifahamisha daktari huyo.

Alifafanua kuwa, endapo mama mjamzito atakosa lishe bora, hata mtoto anapozaliwa anaweza kupata udumavu na utapiamlo, hivyo waandishi wa habari wana wajibu wa kuyazungumzia hayo ili jamii ipate uelewa.

Kwa upande wake mwandishi mwandamizi kutoka PPC Ali Mbarouk Omar alisema kuwa, kuna haja kwa wanahabari kuchukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha wanatumia vyombo vyao kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi.

“Kwa kweli jamii iliyokubwa haijui kuhusu afya ya uzazi na hii inasababisha watu kupata madhara mbali mbali wakati wa ujauzito mpaka kujifungua na mtoto anaezaliwa kuathirika pia”, alisema mwandishi huyo.

Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo walisema kuwa ni kweli kwamba, jamii iliyokubwa haifahamu masuala ya Afya ya uzazi, hivyo kwa kutumia kalamu zao watafanya juhudi kuwaelimisha, ili kuona kwamba madhara yanayojitokeza kwa akinamama hao yanaondoka kabisa.

“Kwanza akinamama wengi hawapati lishe bora na jengine hili la kula vitu visivyosahihi nalo linawaumiza, lakini hawajui kwa sababu huko mitaani wanasema, mjamzito hata ale nini hapati madhara yeyote, jambalo sio sahihi”, walisema waandishi hao.

 

Mapema akifungua mafunzo hayo Afisa Mradi wa Afya ya uzazi kutoka TAMWA Zanzibar Zaina Abdalla Mzee alisema kuwa, lengo la kuwapa mafunzo wanahabari ni kwamba, waelimishe jamii kuhusu masuala ya Afya ya uzazi kwani ni madhara mengi yanayojitokeza bila ya akinamama hao kujitambua.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliandaliwa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na TAMWA Tanzania bara chini ya ufadhili wa shirika la Marekani la WPF.

MWISHO.