Sunday, November 24

Juhudi Zetu Kojani wameomba kukamilishiwa vifaa vya boti waliyopatiwa

NA MARYAM SALUM, PEMBA

KIKUNDI cha uvuvi wa samaki cha ‘Juhudi Zetu’ kilichopo shehia ya Mpambani Wilaya ndogo Kojani, wameiomba Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuwakamilishia vifaa vya boti waliyopatiwa, ili waanze kuifanyia kazi.

Waliyasema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kisiwa cha Kojani, juu ya kujua hatma ya boti ambayo walipatiwa na Serikali hivi karibuni kwa ajili ya kuvulia.

Walisema kuwa, wanahitaji kupatiwa vifaa vilivyobakia ili waanze kuifanyia kazi boti hiyo, jambo ambalo litawafanya watimize malengo yao ya kuzalisha zaidi na kujikomboa kiuchumi.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Mbwana Suleiman alisema kuwa, hivi karibuni Idara ya Uvuvi iliwapatia boti kwa ajili ya kwenda kuvua kwenye maji ya kina kirefu, ingawa bado vifaa havijakamilika, hali ambayo inarudisha nyuma malengo yao.

‘’Serikali ilitupatia boti kubwa yenye uwezo wa kwenda kuvua kwenye maji mengi, lakini tumeshindwa kuitumia kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kuvulia kama vile nyavu na vifaa vyengine’’, alisema.

Kwa upande wake Mshikafedha wa kikundi hicho Omar Abdalla Said alieleza kuwa, wamekuwa wakifanya shughuli zao za uvuvi wa samaki kwenye maji makubwa kwa kutumia vidau (mtumbwi), jambo ambalo linahatarisha maisha yao.

‘’Suala la uvuvi wa samaki katika maji makubwa kwa kutumia mitumbwi sio suala rafiki kwetu, kwani tunahatarisha maisha yetu, lakini kutokana na hali ngumu ya maisha tuliyonayo tunakwenda tu ili tupate fedha ya kutusaidia’’, alisema.

Katibu wa kikundi hicho Siti Shaame Faki alisema kuwa, wanatamani boti hiyo waifanyie kazi ili wafikie mbali kimaendeleo, ingawa hawawezi kufika huko bila ya kukamilishiwa zana za zote zinazohitajika.

‘’Tunaiomba Idara itupatie vifaa ambavyo wametuahidi, kwa sababu wakichelewa hata boti nayo inaweza kuharibika kwa sababu haitumiwi”, alisema Katibu huyo.

Alieleza kuwa, amejiunga kwenye kikundi hicho cha uvuvi kutokana na hali ngumu ya maisha, hivyo ikiwa boti hiyo itakamilishwa vifaa vyake watagomboka kiuchumi, kwani watavua samaki wengi na wakubwa na hatimae kupata fedha nyingi.

Mjumbe wa kikundi hicho Time Mbwana Suleiman aliiomba Wizara husika kufanya wepesi wa kuwapati vifaa ambavyo vinahitajika kama walivyoahidiwa, ili waanze kufanya shughuli zao za uvuvi kwa maendeleo endelevu.

‘’Boti tumekopa, hivyo ikiwa halitumiki tutashindwa kurejesha pesa kwa sababu hatuzalishi, hivyo tunahitaji vifaa tuvipate kwa haraka ili tuanze kazi”, alisema Mjumbe huyo.

Afisa mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Pemba Dk. Salim Mohamed Hamza alifahamisha kuwa, kama walivyopatiwa boti na mashine, basi waamini kwamba na vifaa vilivyobaki vitawafikia ili waanze kazi.

Aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na subra kwani Wizara ina mpango wa wanawapatia vifaa vilivyobaki, ili kuendeleza shughuli zao za uvuvi kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Kikundi hicho kimeanzishwa mwaka huu, ambacho kina wanachama 20 wanaume nane (8) na wanawake 12.

MWISHO.