NA MARYAM SALUM, PEMBA
KIJANA Abdalla Bakari Ali miaka 29 mkaazi wa Amani Road Wilaya ya Chake Chake amefikishwa katika Mahakama maalumu ya kupambana na kesi za udhalilishaji iliyopo Kusini Pemba, kwa tuhuma za kumbaka msichana wa miaka 16.
Wakati mtuhumiwa huyo akiwa kizimbani hapo kusikiliza shauri linalomkabili mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Muumini Ali Juma, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Ali Amour Makame alidai kwamba shauri limefikishwa kwa ajili ya kusomwa.
“Muheshimiwa hakimu shauri linalomkabili mtuhumiwa limefikishwa katika mahakama yako, ili tuweze kumsomea na mtuhumiwa aweze kulisikia, hivyo tunaiomba mahakama iridhie ombi letu tuweze kumsomea,” alidai mwendesha mashitaka huyo.
Mara baada ya ombi hilo kutoka kwa upande wa mashitaka hakimu Muumini hakupinga na ndipo alipomtaka mwendesha mashitaka huyo kuendelea na taratibu za shauri hilo.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa Abdalla Bakari Ali mwenye miaka 29, mnamo Machi 26 mwaka 2022, saa 2:30 usiku huko Dodeani Wilaya ya Chake Chake Kusini Pemba, alimuingilia kimwili msichana mwenye miaka 16, jina limehifadhiwa, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Mapema mwendesha mashitaka huyo akimsomea mtuhumiwa shitaka lake linalomkabili, mtuhumiwa alikataa na kudai kwamba hajafanya jambo na kuomba Mahakama impatie dhamana ombi ambalo lilipigwa na chini mahakamani hapo, na kutakiwa kwenda rumande na kurudi tena mahakamani hapo Agosti 7 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi.
“Hakimu”, shauri lako halina dhamana kwa mujibu wa sheria kifungu 151(1), sheria nambari 7 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar, hivyo utakwenda rumande hadi Agosti 7 utarudi tena mahakamani hapa kujakusikiliza mashahidi,” ilidaiwa .
Ilidaiwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 108(1),(2),(e), na 109(1), vya sheria nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
MWISHO.