NA HAJI NASSOR, PEMBA
WATOTO wa shehia ya Mtambwe kusini wilaya ya Wete, wameachiwa maeneo maalum ya kuchezea wakati wanapokuwa na mampunziko ya masomo au skuli zinapofungwa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wazazi na walezi wa shehia hiyo walisema, wamekuwa wakikumbushana kila wanapojenga nyumba za makaazi, kuacha nafasi maaluma kwa ajili ya watoto wao.
Walisema, watoto wanapokosa sehemu za kucheza karibu na makaazi yao, wanakwenda masafa ya mbali, ambapo usalama wao huwa mashakani.
Mmoja kati ya wananchi hao Ali Abdalla Ali alisema, wamekuwa wakieleza namna ya umuhimu wa watoto kupata sehemu mwafaka ya kucheza.
Mwananchi Jabir Saleh Jabir alieleza kuwa, mtoto anapokuwa na sehemu nzuri ya kucheza, hupata uchangamshi wa akili na mwili, jambo ambalo humpelekea kukua vizuri.
‘’Mtoto anahitaji muda wa kuchezea, tena kwenye eneo lililosalama, vyenginevyo atakuwa mbali na makaazi yao na anaweza kukumbwa na majanga,’’alieleza.
Kwa upande wake, mzazi mwenye watoto tisa Mafunda Abdalla Omar wa kijiji cha Mkanjuni alisema, ni lazima kwa wananchi wanapoanzisha majengo, kuhakikisha wanaweka maeneo ya kuchezea watoto.
‘’Mtoto baada ya kurudi masomoni, anahitaji kuchanganyika na wenzake na hivyo ni lazima apate muda wa kucheza, ili akili itanuke’’alieleza.
Nae mzazi Neema Abdalla Omar, aliwashauri wazazi na walezi wenzake, kuwaruhusu watoto wao kushirikiana na watoto wengine katika kuchangamshana kimazingira.
‘’Pamoja na uwepo wa changamoto za majanga mbali mbali, lakini bado watoto wanayo haki ya kupewa muda wa kucheza na kuchanganyika na wenzao’’, alifafanua.
Mtoto Hilmin Issa Othman alisema, pamoja na uwepo wa maeneo ya kuchezea, lakini baadhi ya vijiji kumekuwa na ujenzi usiofuata tararibu.
Mtoto Mayasa Haji Omar na Aisha Mkuu Hashim walisema, mkazo zaidi uwekwe kwa wazazi na walezi katika kuwalinda na majanga mbali mbali.
‘’Kwa maeneo ya kuchezea katika shehia yetu ya Mtambwe kusini yapo, lakini sasa wazazi waungane kutulinda na majanga kama ya udhalilishaji, ambayo wakati mwengine hufanywa na watu wa karibu’’, walishauri.
Mapema Sheha wa shehia Mtambwe Kusini wilaya ya Wete Othman Ali Khamis alisema, amekuwa akishirikiana na wajumbe wa kamati yake, kuhakikisha wananchi wanapojenga wanabakisha maeneo ya kuchezea.
Alisema, maeneo hayo pamoja na kutumiwa na watoto, hata jamii inapokuwa na shughuli zake kama misiba, harusi na shughuli za kiserikali nayo hutumia.
‘’Wananchi kwa kiasi fulani wamekuwa wakiangalia suala la kuacha maeneo ya wazi ‘open space’ kwa ajili ya watoto kucheza karibu na makaazi yao’’, alifafanua sheha huyo.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuongeza kasi ya ulinzi wa watoto wao, kwani wanakumbana na majanga hata wanapokuwa katika makaazi yao.
Mwisho