NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
WANAFUNZI 720 wa skuli ya Msingi Chwaka wilaya ya Mkoani Pemba, wameanza kusahau kujisaidia vichakani, kama ilivyokuwa zamani, bada taasisi ya Ifraji Zanzibar Foundation kuwajengea matundu 12 ya vyoo.
Kati ya matundu hayo, mawili kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitajia maalum, na 10 ni kwa ajili ya wanafunzi wengine wanaosoma skulini hapo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vyoo hivyo, vyenye thamani ya shilingi milioni 25,000 Mratibu wa taasisi ya hiyo kwa upande wa Pemba Abdalla Said Abdalla, alisema taasisi hiyo imeamua kuondosha tatizo hilo kwa wanafunzi, kujisaidia vichakani.
Alisema hapo awali wanafunzi wa skuli hiyo walikua wakipata shida wakati wakwenda kujisaidia, hali iliyokua ikiwalazimu baadhi yao kwenda kujisaidia vichakani, jambo ambalo lilihatarisha afya zao.
Alisema, jukumu la Ifraj ni kusaidia jamii kuondokana na umasikini na kutatua changamoto za elimu, katika maeneo mbali mbali, ili watoto wasome katika mazingira mazuri.
“Baada ya kuona wanafunzi wako katika mazingira hatarishi kwa kujisaidia vichakani, tumeamua kuwasaidia ili waepuke maradhi ya mripuko,’’ alisema.
Akizunguzia suala la vitendo vya udhalilishaji, Mratibu huyo aliwataka wazazi na walimu kupiga vita vitendo hivyo, kwa kuwasimamia vizuri watoto, katika mazingira ya majumbani na masomoni.
Hata hivyo aliushauri uongozi wa skuli hiyo na Wizara ya Elimu, kuhakikisha wanavitunza vyoo hivyo, ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuviweka katika hali ya usafi.
Mwenyekiti wa kamati ya skuli hiyo Khalfan Massoud Khamis, alisema mradi huo, umefika kwa wakati muwafaka, kwani skuli hiyo ilikuwa na uhitaji mkubwa wa vyoo.
“Kipindi cha mvua watoto wanazidi kupata usumbufu, kwa kweli hili limeleta faraja kwetu, tutavitunza ili vidumu,’’ alisema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Afisa Majengo kutokaWizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Pemba Salim Abdalla Kabi, aliishukuru taasisi ya Ifraji kwa msaada huo, kwani hapo awali walikua na upungufu wa vyoo katika skuli hiyo.
Alisema, choo kimoja kilikuwa kikitumiwa na wastani wa wanafunzi 100 na wengine kujisaidia vichakani, ambapo sasa wamepata vyoo 12 kila tundu moja litatumiwa na wanafunzi 60 na vyoo viwili vya mahitaji maalum.
Nae Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Chwaka Kassim Ibrahim Mussa, alisema taasisi hiyo imefanya jambo kubwa, katika sekta ya elimu kwa kuwapatia vyoo vya kisasa.
Hata hivyo aliwaomba wadau mbali mbali wa maendeloe na serikali, kujitokeza kuwapatia msaada wa vyoo vyengine, ili wanafunzi waweze kujisaidia katika mazingira mazuri.
Nae Mratib wa Afya ya Mazingira kutoka Wizara ya Afya Pemba Daktari Khalfani Shaaha, alisema tundu moja ya choo linahitaji kutumiwa na wanafunzi 40 wanaume na 45 kwa wanawake, kuwepo na choo cha watu wenye mahitaji maalumu, choo cha viongozi wa skuli hiyo.
Shirika la Afya Duniani kwenye ripiti zake, linaanisha kuwa, tundu moja ya choo, ni kwa wanafunzi 25, ingawa muongozo wa wizara ya Elimu Zanzibar wa mwaka 2016, unatambua kuwa, tundu moja la choo ni kwa wanafunzi 40 hadi 45.
Taarifa ya wizara ya Elimu Zanzibar, imeeleza kuwa, katika mwaka uliomalizika, wizara imekamilisha ujenzi wa vyoo 525, Unguja 281 na Pemba 244, kupitia mradi wa UVIKO 19 na misaada ya wahisani mbali mbali.
MWISHO