Monday, November 25

AFYA YA UZAZI SALAMA KWA WANAFUNZI WAKIKE INAHITAJI MAZINGIRA SALAMA KIPINDI CHA HEDHI

AMINA AHMED MOH’D, PEMBA. 

Hedhi salama ni hali ya Mwanamke au msichana aliye katika hedhi kuwa na uwezo wa kupata kifaa salama na nafuu cha kuzuia Damu, kupata Maji Safi na salama ya kujisafishia, kuwa na maliwato yenye mlango kwa ajili ya kujisitiri na kubadilishia vifaa vyake pia kupata sehemu sahihi ya kutupa au kutunzia kifaa chake baada ya kukitumia   
KAMA Hiyo ndio maana halisi ya Hedhi salama bila shaka Bado kuna mengi yanahitaji kuangaliwa na wadau Serikali na wote wanaopenda Maendeleo Bora ya Afya ya Uzazi na  Elimu kwa watoto wa kike. 
 
Wadau wengi hujali  Afya ya mtoto wa kike kwa kutoa  Elimu  ya Afya ya Uzazi kwa baadhi ya wanafunzi waliofikia  Umri wa Kupata Hedhi kwa  kugawa Sabuni pamoja na Taulo zakike lakini bado kuna changamoto Nyingi ambapo zisipoangalia kwa jicho la Tatu na Wadau pamoja na Serikali kwakuwekewa mkakati Endelevu Kugawa Taulo kutoa Elimu na Sabuni hizo  hautokuwa Msaada kwa Wanafunzi Wakike Maskulini bali kutaendelea kuhatarisha hali Za Afya zao na kuleta Athari baadae. 
Jee ni kwa namna gani yataweza kufikiwa Maendeleo ya Elimu ambayo itakuja kuwa mkombozi baadae katika Maisha ya mtoto wa kike ni pamoja na kuwa na Afya imara Mazingira salama na upatikanaji wa huduma muhimu ambazo zitasaidia kuondosha usumbufu wanapokuwa katika kipindi cha Hedhi.
Wanafunzi wengi wakike ambao wamefikia umri wa baleghe ( kuvunja ungo) wakiwa katika harakati za kutafuta Elimu.
Wapo wanaolazimika kukaa katika madahalia ili kuona ndoto ya kupata elimu bila usumbufu ,lakini pia wapo ambao hulazimika kuwekewa mazingira maalum ambayo yatawarahisishia upatikanaji wa Elimu kwa kukaa katika nyumba maalum kujisomea.
Huduma Muhimu ambazo zinaulazima katika kufikia afya bora ya Mwanafunzi wa kike ni pamoja na Kuwepo na mazingira rafiki  ya kutumia wanapokuwa katika kipindi hicho cha Hedhi.
Changamoto hizo ndizo ambazo zimenifanya niandae Makala hii maalum ambayo itasaidia kukumbusha serikali wizara ya Elimu pamoja na wadau  wa maendeleo ya mwanafunzi wa kike kuhusu kadhia hizi ambazo endapo hazitoangaliwa kwa jicho la tatu huenda hedhi salama ikaendelea kubaki kwa maneno bila uhalisia kwa wanafunzi wa kike.
Mazingira hayo ni pamoja Huduma ya maji safi   vyoo salama, ,elimu kuhusu afya ya viungo vya uzazi kwa mwanamke,vyumba vya kujisitiri na kuvaa nguo, kupatikana kwa Taulo za kike kwa wakati mazingira maalum ya kutupia Taka (Jaa).
” Skuli yetu inaukosefu wa Huduma ya Maji hususan ni Sisi ambao tunakaa katika  Dahalia hili la hapa Nje ya Skuli,  Jambo ambalo linapelekea  kutumia Maji kwa umakini kutokana na Upungufu huo hivyo,  Usafi Unapungua, Maradhi yanajitokeza  Wengine wameanza Kupata Maradhi ya Ngozi,  Vyoo  havifanyiwi Usafi wa kutosha tunahofia kupata Maradhi Ya UTI,  Ni maneno ya Mwanafunzi Asma Ameir Khamis, Awena Khamis Ali, Pamoja na Faidhat Adam Kombo baadhi ya  wanafunzi wanaosoma na kukaa katika Dahalia Skuli ya Sekondari Madungu Chake Chake.
 “Ni Afadhali Wanaotoa misaada Watupigie Kelele Kupata Maji Ya kutosha  katika Skuli yetu Kwa sababu  Nasubutu kusema kuwa Kipindi Cha Hedhi kwetu bila maji ya kutosha ni Uchafu Zaidi Vyooni, jambo ambalo ni Athari kwa afya Zetu sisi watoto”    Aisha Omar Abdalla Mwanafunzi kidato cha Tano Madungu Sekondari.
 “Hatuna Dampo Skulini kwetu tunalazimika Kuweka Pale  katika  Madude ya kuhifadhia Taka Ili Watu wa Usafi wa Baraza waje kuchukua Siku nyengine inafika Siku tatu hawajaja  Uchafu  Unakaliana Tunaiomba Serikali Kuliangalia Suala Hili”.

Baadhi Wanafunzi wa kike wanatumia Matambara wakati wa Hedhi kutokana na kutoweza kumudu Bei Ya Taulo Baadhi ya Wanafunzi Huku wengine Tukiona kama ni Ugonjwa Ambao kwa Tamaduni zetu kumueleza  Baba au mama Tunaisikia Aibu sana, kwa kweli, inaskitisha mno kwani Matambara hayo yanaweza kuacha Madoa ya hedhi kwenye nguo zetu za Skuli Pamoja na nguo za ndani”. Alidai Fatma Abdalla Mbarouk Kutoka skuli ya Sekondari  Msuka.

” Wahisani Waliangalie na Suala la Maji katika skuli yetu ya Msuka Sekondari Wanafunzi wa kike Tunapitia changamoto Kipindi cha Hedhi, na naamini sio Skuli yetu peke na yengine pia” Ruwaida Salum Hamad Mwanafunzi Msuka Sekondari  Wilaya ya Micheweni.

” Bado Tunadhana potofu juu ya Suala la Hedhi  binafsi Sijawahi kuumwa na Tumbo  la hedhi nikamwambia Mzazi wangu wa kiume Na hata mama naona ugumu sana hulazimika kuja Skuli na Maumivu yangu nikifika Siwezi kusoma wala sikai kwa utulivu ila inanibidi nikae hivyo Tunaiomba Serikali iweke suala hili la Afya ya uzazi kuanzia madarasa ya nne ambapo wanawake wengi huanza kupata baleghe”  Thuwaiba Juma Muhammed Skuli ya Sekondari Chambani Kusini Pemba.
 “Mimi naona Ninapokuwa katika  siku zangu Kwanza nakuwa kama nina maradhi ya kuenda Chooni mara kwa mara, Huku naona kama nadhuriwa na vyakula na maji kwa sababu nakuwa nafanya kama ugonjwa wa ngozi mwilini kila ninavyitumia Maji naona hayatoshi Nakuwa na wasi wasi mkubwa   na Mazingira  Ya kutupa Pedi Nahofia  Sababu Vyoo ni vichache Ukilinganisha na wanafunzi Tuliopo hapa Pindua tupo kuanzia Kidato cha Kwanza “Zubeida Amour Skuli ya Sekondari Muhammed Juma  Pindua.
 Nasubutu kusema wazazi Sijui tumewalea kwa kutokiwa wawazi watito wetu wakike Lakini Hili suala kwao wamekuwa kama ni aibu au siri ambayo wanahisi mzazi hastahiki kujua hususan ni sisi Akina baba, Binafsi mimi nina watito wakike wakubwa lakini kama sio mama yao kuniambia wao hawajawahi kuniambia masuala hayo kabisa  , Wito wangu Tubadilike Alisema Muhammed Salum Mzazi Madungu.

Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Muhammed Nassor Salum amesema  kuwa licha ya jitihada za Serikali na wadau bado tatizo la Hedhi Salama  Skulini  linahitaji Mikakati Endelevu,  kutokana na Umuhimu wake  .

“Wizara ya Elimu inafanya  Jitihada  mbalimbali ikiwemo kuimarisha Miundo mbinu kuwa Rafiki kwa watoto wakike,  Kutumia vyumba maalum wanapokuwa katika Vipindi vya Hedhi, waalimu washauri ,  Taulo  zinakuwepo Mashuleni Maji lakini  bado inakuwa havijitoshelezi kwa vile suala hili ni endelevu  kwaio Tunaendelea na namna bora ya kuliangalia suala hili  katika mikakati endelevu  Ili kuona  watoto wakike hawakosi masomo wanapokuwa katika Mzunguko.

Kwa Mujibu  Waziri wa Afya Tanzania  Ummi Mwalim  Asilimia 48 ya wanafunzi wa kike wanakosa Masomo kutokana na kuwa katika mzunguko wa Hedhi hali ambayo huathiri uwezo wa wanafunzi hao kujifunza kwa ufasaha.
Takwimu zilizofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu kwa kushirikiana na Maabara ya Afya ya Jamii Pemba  uliowafikia  wanafunzi wakike kwa Asilimia 78  katika  mahojiano ndani ya  Skuli  294  Katika Mikoa 19 Tanzania Bara na Zanzibar ambapo utafiti huo Ulionesha kuwa Asilimia  48, ya Wanafunzi Waliohojiwa  walisema kuwa  huathirika na kupoteza uwezo wao wa kujifunza kutokana na Sababu mbali mbali ikiwemo Maumivu ya Tumbo , Kukosa Taulo, Maji na Mazingira rafiki wanapokuwa Skuli.

Ikumbukwe kuwa kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira kupitia Mpango Endelevu ya Maji na Usafi wa Mazingira Skuli na  vijijini Mwaka 2020/21, ilieleza kuwa  Serikali ya  Tanzania imeweza kujenga Miundo mbinu ya vyoo vikiwemo vya Wanafunzi wenye ulemavu pamoja na sehemu ya Hedhi salama ambayo ina vifaa muhimu vinavyohitajika katika shule 835 kwenye Mikoa 17 pekee.

Aidha Kwa Mujibu wa Taarifa iliyitolewa na Ofisi ya Takwim Tanzania  (NBS) juu ya masuala ya Maji na usafi Mazingira  skulini mwaka 2018 inaonesha asilimia 66.8 ya shule ndizo zina huduma ya Hedhi salama ambapo kati ya hizo zilizobainika kuwa na viteketezi ni asilimia 24 huku asilimia 22.8 zinatupa taka kwenye mashimo na 19.5 zina vichomea Taka visivyokidhi.

Hata Hivyo kwa Visiwa vya Unguja na Pemba Serikali  Ya Mapinduzi kupitia Wizara ya Afya  Kitengo Cha Lishe  Kilifanya Utafiti Mdogo Mwaka 2022  karika skuli mbali mbali Na kubaini kuwa Asilimia 25 ya  Mahudhurio ya Skuli kwa  Wasichana wakati Hedhi, hawahudhurii ioasavyo, huku Ikibainisha kuwa Asilimia 12.5 wakihudhuruia bila kuwa na Usomaji mzuri kutokana na sababu mbali mbali za Kiafya.

JEE  UTI NI NINI?

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Makala hii walieleza hofu yao  juu ya Kupata Maradhi ya  UTI

UTI kwa Wanawake ni maambukizi ya Mfumo wa Mkojo kwa wanawake ambao huhusisha figo, kibofu cha mkojo  Mrija wa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo  pamoja na mrija unao unganisha figo na kibofu cha mkojo,Ambapo Mambukizi haya kwa kiasi kikubwa husababishwa na Bakteria Jamii ya    Escherichia( E.coli), ambao moja kwa moja huathiri Mfumo wa Mkojo, Na Wanawake Huweza kupata Hatari ya  Maambukizi haya endapo atakuwa katika hali zifuatazo,    Kinga ya mwili kutokuwa imara, Kutumia vifaa au dawa za kuzuia mimba, Kupungua kwa homoni ya Estrogen, Ugonjwa wa kisukari,  Kufanya ngono isiyo salama, Mimba, Pamoja na  Kutumia choo kichafu.

Mwanamake huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuugua ugonjwa huu pamoja na kujirudia mara kwa mara kwa kuwa mrija wa mkojo huwa ni mfupi sana tofauti na mwanaume, pia tundu la uke huwa karibu na sehemu ya haja kubwa hivyo ni rahisi kwa Bakteria kutoka kwenye Choo kuingia ukeni jambo ambalo husababisha kuongezeka kwa Matumizi ya Vyoo mara kwa mara kutokana na Kupatwa na maumivu wakati wa haja ndogo, Kujisaidia haja ndogo mara kwa mara isiyotoa mkojo mwingi, Kujisaidia mkojo mweusi au ulio na chembechembe za damu na harufu kali, Maumivu ya nyonga, Uchovu, Homa na kutapika, Maumivu ya sehemu ya chini ya tumbo.

Alphonce  Mbarambe Gura  ni Mwanasheria kutoka  Taasisi ya Legal Service  Facility  Zanzibar alisema kuwa Suala La Hedhi  linatambulikana  kikatiba  kama ni haki ya Msingi kati ya  Haki za Binaadamu kwa vile suala  hilo linagusa moja kwa moja Utu.

“Lazima suala la Hedhi Salama liangaliwe kwa upana wake hivyo ni lazima Watoto wakike wenyewe  waweze kujua ni jinsi gani suala la hedhi Salama ni muhimu kwao, haki ya kupata vifaa vya kujisitiri kwa gharama nafuu ambavyo ni salama , kupata Mazingira wezeshi Skuli na Nyumbani ya kubadilishia nguo Maji  ya  Salam kwa vyovyote hivi wanayo haki ya kudai  endapo watakuwa Skuli  ama Majumbani ni haki inayitambulika kisheria Hedhi ni Haki ya Utu, Utu unatakiwa kuthaminiwa wito wangu wanafunzi waamke kusoma kujua haki zao na waweze kuzidai kisheria”.

Mwache Juma Abdalla ni  Mwalimu Mkuu skuli ya Conecting continent Sekondari anasema  Wanafunzi waliowengi Hukosa   Furaha  na hamu ya kusoma  Wanapokuwa katika kipindi Cha Hedhi kutokana na  Sababu mbali mbali jambo ambalo uongozi wa Skuli hiyo kutumia Umakini Mkubwa ikiwemo masomo ya  Muda wa ziada, katika Kufundisha ili kuepusha ufaulu  mbovu kwa Wanafunzi wa kike.

Mtumwa Said Khamis Ni Mwalimu Mshauri  na nidhamu Skuli ya Madungu Sekondari anasema “Mara chache sana na Wanafunzi   ndio hunifuata Kueleza Changamoto wanapopatwa na dharura  hiyo, Tunatumia uzoefu wetu kugundua hizo changamoto na kuwasaidia hawasemi.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar Kupitia Mradi wa Afya ya Uzazi wamesema Changamoto Zinazokabili Wanafunzi juu ya Masuala ya Hedhi Salama kwa Wanafunzi wamesema Wanazipatia Ufumbuzi kwa Kuandaa Elimu maalum kwa Waandishi wa Vyombo mbali mbali na kueleza  Athari  ili Jamii na wahisani mbali mbali waweze kuzibaini na kuzipatia Msaada wa Haraka.

Kama ambavyo Taasisi mbali mbali zimekuwa zikiendelea kutoa msaada wa Taulo za kike kwa baadhi ya wanafunzi kadhalika Serikali na Wadau iliangalie suala hili la Elimu, Maji, Vyoo  vya Matundu, pamoja Na Majaa (Dampo) ,  Uoatikanaji wa Taulo za kike kwa wote kwa garama nafuu, ili kuimarisha Zaidi Afya ya Hedhi salama Kwa wanafunzi wa Kike  kwa vitendo .

Mwisho.