AMINA AHMED MOH’D, PEMBA.
ZAIDI ya Viongozi 15 kutoka vyama mbali mbali vya Siasa kisiwani Pemba wamepatiwa Mafunzo maalum kujengewa uwezo juu ya Kuanzisha na kuifanyia kazi Sera ya jinsia Katika Vyama Vyao.
Mafunzo hayo ya Siku moja yaliondaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Jumuia ya Utetezi wa kijinsia na Mazingira Pemba PEGAO yamefanyika Leo katika ukumbi wa Chama hicho Mkanjuni Chake Chake.
Akizungumza katika Mafunzo hayo Mratibu wa chama hicho Pemba Fat-hiya Mussa Said Amesema lengo la Mafunzo hayo kwa Viongozi wa vyama vya Siasa ni kusaidia Kuongeza ushiriki wa wanawake Katika Demokrasia kwa kufuata Utaratibu maalum utakaotambulika kisheria, kusimamiwa pamoja na kuweza kutekelezwa kupitia Sera ya Kijinsia ndani ya Vyama.
” Baada ya kuona Changamoto kubwa ndani ya Vyama vya Siasa ni kukosekana kwa Sera ya kijinsia, na Vile ambavyo vimebahatika kuwa na Sera basi haviitekelezi Tukaona ipo haja ya kuandaa Mafunzo haya ili kupeana miongozo jinsi gani tunaweza Kuandaa Sera ya jinsia ambazo zitasaidia Kupatikana usawa kwa Wanawake na wanaume katika Vyama”Alisema.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Jumuia ya Pegao Hafidh Abdi Said amewataka viongozi hao kuyafanyia kazi kwa vitendo Mafunzo hayo ili kuweza kuleta matokeo chanya katika vyama vya siasa ambayo yatatokana na kuanzishwa kwa sera ya jinsia ambayo imezingatia usawa wa Kijinsia na ushiriki na upatikanaji wa fursa sawa kwa vitendo.
“Haya mafunzo malengo yake ni kupata Mabadiliko ndani ya vyama tunahitaji zile changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wanawake zilizomo ndani ya vyama vya siasa zinazowarudisha nyuma kugombea uongozi zisijitokeze tena”.
“Turudi katika jamii zetu tukashauriane tuwashirikishe ili kuona ni kwa namna gani vyama vyetu vinakuwa na sera ya kijinsia , isiwe Maneno matupu tunataka mabadiliko kuona wanawake na wao wanapata fursa ya kugombea uongozi kwa Miongozo ya kisera iliyomo ndani ya vyama”alisema Mkurugenzi Pegao.
Sabah Mussa Said ni mkufunzi katika mafunzo hayo pamoja na mambo mengine amesema Kupatikana kwa Sera ya kijinsia katika vyama vya siasa kutasaidia kuondosha ubaguzi na unyanyasaji wa aina zote ambao hujitokeza kutokana kukosekana au kushindwa kupewa vipaumbele kwa sera hizo ndani ya yyama .
Wakizungumza baadhi ya viongozi walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Muhammed Haji Kombo Mwenyekiti Wa chama cha wananchi CUF Mkoa wa Kusini Pamoja na Hamiar Ali Said kutoka chama hicho Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema chama kitaendelea kulinda na kuendeleza haki na upatikanaji wa fursa sawa kwa Wanawake na wanaume.
Raya Juma Othman pamoja na Rufea Muhammed Saleh Viongozi kutoka chama cha wakulima AFP wamesema katika kuona wanawake wanapata fursa sawa katika kushiriki michakato ya uongozi wataendelea kuyafanyia kazi mafunzo hayo ya Sera ya kijinsia kwa kushirikiana na Viongozi wa juu zaidi ndani ya chama chao kuanza mara moja mchakato wa kuanzisha Sera ya Kijinsia.
Mafunzo hayo ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyama mbali mbali vya siasa yalitoa fursa ya kushiriki kwa Pamoja katika kuitolea Ufafanuzi mada ya Sera ya jinsia katika vyama vya Siasa.
Mwisho.