NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
MKUU wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, ameitaka Kamisheni ya Ardhi Pemba, kuharakisha utoaji wa hati ya matumizi ya ardhi kwa wananchi, ili kuondoa migogoro inayojitokeza katika jamii.
Alisema utolewaji wa hati hizo, utasaidia kuondosha migogoro ya ardhi inayotokea katika jamii, pamoja na kuwasaidia wananchi, kuzitumia katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo.
Mkuu huyo wa wilaya aliyaeleza hayo, wakati wa hafla ya ugawaji wa hati ya haki ya matumizi ya ardhi, kwa wananchi wa shahia ya Gombani wilayani, hafla iliyofanyika uwanja wa mpira Gombani.
Alisema, ni vyema kwa Kamisheni ya Ardhi, kukamilisha hati hizo kwa shehia, ambazo wameshazifanyia utambuzi, kabla ya kuingia shehia nyingine, ili kurahisisha wananchi kuzipata kwa wakati.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya alisema, lengo ni kuwapatia wananchi fursa ya kujikwamua kwenye mahitaji ya kifedha, katika taasisi baada ya kua na hati za maeneo ambayo wanamiliki.
“Suala la migogoro ya ardhi, limekua changamoto katika maeneo mengi, na ardhi tulionayo haiongezeki zaidi ya kupungua na mahitaji yameongezeka migogoro inatokea,”alisema.
Aidha aliwataka wananchi wa shehia ya Gombani ambao bado hawajakamilisha taratibu kukamilisha, ili lengo la serikali kuhakikisha ardhi yote inapimwa na kufanya uharaka wa kutoa hati hizo.
Aliwapongeza wananchi wa shehia ya Gombani kukamilisha taratibu za malipo, kila mwananchi kupatiwa hati ya haki ya matumizi ya ardhi, ili malengo na mipango iweze kufanikiwa.
Nae Kaimu Afisa Mdhamini wizara Ardhi na Maenedeleo ya Makaazi Pemba Khamis Hamad Iddi, alisema hati hizo zitawasaidia wananchi, kuwainua kiuchumi kupitia ardi zao.
Mapema Naibu Mrajisi wa Ardhi Pemba Asha Suleiman, alisema ardhi iliyosajiliwa, na kutambuliwa inapunguza migogoro, na inamsaidia mwananchi kiuchumi kwa kupata mikopo katika taasisi za kifedha.
“Sote ni mashahidi, kuna taasisi za kifedha zinatoa mikopo kwa lengo la kusaidia wananchi kiuchumi, mradi unawataka wananchi ardhi isitumike kuendeleza jina la ukoo, pia ardhi iwasaidie kiuchumi kwa kupata mikopo,”alisema.
Aidha alisema utambuzi wa ardhi Zanzibar ulianza mwaka 2009 kupitia mradi wa Mkurabita na mradi wa SMALL II, ambapo kwa wilaya ya Chake Chake shehia ya Wara na Mkoroshoni na hati walishapatiwa.
Alisema katika shehia ya Gombani, tayari wameshafanya kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ni hati 159 zitatolewa na awamu ya pili ni hati 200 ambazo kwa sasa ziko katika hatua ya kusainiwa ili zikabidhiwe kwa walengwa.
Akizungumzia changamoto ya zoezi hilo, ni wananchi kulihusisha zoezi hilo na ukusanyaji wa wa ardhi, hali inayopelekea ugumu kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa shehia ya Gombani, sheha wa shehia hiyo Subira Abdalla Juma, ameishukuru Kamisheni ya Aridhi, kwa kuwapatia hati hizo, ambazo zitaweza kuwasaidia katika mambo yao mbali mbali ya kijamii.
Mpango huo wa utambuzi wa aridhi unatekelezwa na Serakali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kupitia mradi wa mkurabita pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
MWISHO