NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
WANANCHI wa kijiji cha Andikoni shehia ya Chumbageni wilaya ya Mkoani, wamesema wakati umefika kwa kijiji chao, kuanza kunufaika na matunda ya serikali ya awamu ya nane Zanzibar, ikiwemo barabara ya kisasa.
Wamesema kijiji hicho tokea kuasisiwa hadi hasasa, hakijawahi kuwa na huduma yoyote ya kijamii, ambayo wananchi wanaweza kuipata kama ilivyo kwa vijiji vyengine.
Hayo yamaebainika katika mkutano wa kusiliza kero za wananchi, ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na kufanyika kijijini hapo.
Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake Mohamed Juma, alisema ukosefu wa barabara kijijikwao umepelekea huduma zote muhimu kokosekana, ikiwemo elimu, afya, maji na umeme, hali inayowafanya baadhi ya akinamama kujifungulia njiani.
Alisema suala la elimu, watoto wanalazimika kutembe kilomita mbili, kutoka Andikoni hadi skuli iliko, huku wakipita kwenye mapori hali inayowatia hofu baadhi ya wazazi.
Kwa upande wa huduma za afya, alisema wananchi hulazimika kuzifuata kituo cha afya Wambaa au Mtambile, jambo ambalo linarudisha nyuma hata wazazi, kuona uzito kuwapeleka watoto wao skuli.
“Sisi hapa kama tunahitaji kujaza chaji simu zetu mpaka tufike kijiji cha jirani tukaombe na ikijaa mtu anarudia nayo, huu ni usumbufu na sisi tunataka kuangalia taarifa za maendeleo ya nchi yetu,”alisema.
Nae mwanakijiji Mohamed Khamis, alisema kipindi cha mvua kijijini kwao, hakuna kitu kinachoingia wala kutokana, kutokana na barabara yao ilivyoharibika.
Kwa upande wake Tatu Juma Haji, alisema wanakumbana na changamoto kubwa ya kujifungulia njiani, kutokana na ukosefu wa barabara kijiji kwao, pamoja na umbali wa vituo vya afya vilipo.
“Sisi hapa urahisi bora mtu apitie baharini hadi hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, kwa huku kwetu utazaa njiani, kwani tayari matukio hayo yameshatokea,’’ alisema.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema kwa hatua ya kwanza, barabara hiyo itasafishwa, ili iweze kupitika wakati wote na ujenzi wa barabara za ndani, utakapofika basi nayo kutengenezwa .
Nae mkuu wa Idara ya Ufundi wa Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’ Pemba Mohamed Ali Juma, alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 watahakikisha huduma ya umeme, inafikishwa kijijini hapo.
“Huku lazima tuweke tansfoma ili huduma iweze kupatikana kwa urahisi, lazima uvuke kupitia baharini na tutahakikisha huduma itafika, iwapo barabara itakua nzuri,”alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Maji Zanziba ‘ZAWA’ Juma Omara Khamis, alisema tayari walishawasiliana na taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, kwa ajili ya kuwasaidia kisima na ZAWA kujenga mnara wa tenki la lita 10,000 ili wananchi wanaondokane na shida ya maji.
Mwakilishi kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Salum Kuza Sheikhan, alisema kijiji hicho wamekipa kipaumbele, kwani watahakikisha banda linalojengwa na tutu linamalizwa na wizara husika.
Akizungumza kwa niaba ya wizara ya Afya, daktari Haji Bakar, alisema wataongeza huduma za mama na mtoto kupitia watoa huduma wao wa vijijini, ili wajawazito kupata huduma ipasavyo.
Mapema mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, aliwataka wananchi wakijiji hao kujenga imani na viongozi waliofika katika kutatu changamoto zao.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema dhamira ya serikali ya awamu ya nane, ni kuona wananchi wanapata huduma bora, ikiwemo elimu, afya, maji safi na salama, pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafiri.
Alisema suala la barabara ni muhimu atahakikisha ujenzi wa barabara ya Wambaa itakapofika na njia zote za ndani zitaweza kutengenezwa, kwa kiwango cha lami.
Kijiji cha Andikoni shehia ya Chumbageni kina wastan wa nyumba 52 na wakaazi 477, huku shughuli kuu za wananchi wa kijiji hicho uvuvi, kilimo na ufugaji.
MWISHO