Monday, November 25

Washauriwa kuyatumia maonesho ya elimu ya juu kujifunza

AFISA Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, akisalimiana na Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Pemba Dr.Ernest Haonga, katika ziara ya kuangalia maonesho ya vyuo vya Elimu ya juu Gombani Wilaya ya Chake Chake.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
MKUU wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Pemba Dr.Ernest Haonga, akitoa maelezo ya Chuo hicho kwa Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, wakati alipotembelea banda la chuo hicho katika maonesho ya vyuo vya Elimu ya juu Gombani Wilaya ya Chake Chake.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
AFISA Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau (kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Pemba Dr.Ernest Haonga, juu ya kuboresha mfumo wa uwekaji wa taarifa mbali mbali za wanafunzi, uliotengenezwa na mwanafunzi wa chuo hicho jinsi gani uweze kusaidia chinini.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
AFISA Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau (kulia) akiangalia mfumo wa uwekaji wa taarifa mbali mbali za wanafunzi, uliotengenezwa na Mwanafunzi Mansour Juma Khamis kada ya ICT kutoka chuo cha kumbukumbu ya Mwalim Nyerere Tawi la Pemba vyuo vya Elimu ya juu Gombani Wilaya ya Chake Chake.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WAZAZI, Walezi na Wanafunzi wametakiwa kutumia fursa zilizopo katika maonesho ya vyuo vya elimu ya juu, yanayoendelea katika viwanja vya Gombani Pemba, ili kupata taarifa sahihi za vyuo wanavyohitaji kujuinga.

Wito huo umetolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, alipokua akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kutembelea mambanda ya maonesho ya vyuo hivyo.

Alisema ni jambo la busara kwa wanaotaka kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, kufika na kupata taarifa moja kwa moja na sio kusubiri au kusikia kutoka kwa watu wengine.

Alisema wataalamu mbali mbali wapo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Pemba, kwani imeonekana kunashida wakati wa kujiunga na vyuo hivyo fursa iliyopo inapaswa kutumiwa.

“Naishukuru Wizara ya Elimu Zanzibar kupitia taasisi iliyoandaa maonesho haya, ambapo wataweza kuwasaidia vijana wetu ambao walikua wakipata shida wakati wanapotaka kujiunga na vyuo sasa fursa ipo hapa nyumbani,”alisema.

Akizungumzia mfumo wa kukusanya taarifa za wanafunzi ulitengenezwa na mwanafunzi wa fani ya ICT kutoka Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Pemba, aliushauri uongozi wa chuo hicho, kuuboresha zaidi mfumo huo kwani utaweza kusaidia katika skuli na vyuo mbali mbali vilivyopo kisiwani hapa.

Alisema fani hiyo ni moja ya fani muhimu kwa sasa, hivyo aliwataka vijana kujiunga na chuo hicho ili watakapomaliza wataweza kujiajiri wenyewe na sio kusubiri ajira kutoka serikalini.

Aidha alimtaaka mkuu wa chuo hicho baada ya mfumo huo kukaa sawa, kwanza kumfikishia Afisa Mdhamini Wizara ya elimu, ili waweze kuutumia katika skuli zao kwa lengo la kuachana na uhifadhi wakumbukumbu katika makaratasi.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Tawi la Pemba Dr.Ernest Haonga, alimshukuru afisa mdhamini huyo kwa mawazo yake, katika kuhakikisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za wanafunzi unakua bora na unafanya kazi.

Aidha aliipongeza Wizara ya Elimu Zanzibar kupitia kitengo cha elimu ya juu, kwa kuandaa maonyesho hayo kwani ni msaada mkubwa sana kwa wanafunzi katika kufuatilia fani gani anayotaka kusoma katika elimu ya juu.

Alisema mwanafunzi atweza kujua chuo kwa ufasaha zaidi, muda gani anaweza kwenda kujiunga na hicho chuo pamoja na sifa za hiyo fani anayoitaka.

“Bahati nzuri zipo mpaka mamlaka zinazozibiti ubora wa elimu ya juu, wanafunzi watapata nafasi ya kujua chuo gani na fani gani zilizopitishwa na mamlaka husika,”alisema.

Hata hivyo, alisema wanafunzi wanaosoma katika chuo cha kumbukumbu ya mwalimu nyerere, wanafursa ya kuajiriwa katika maeneo yoyote nchini Tanzania, kutokana na umahiri wa chuo hicho.

Kwa upande wao wanafunzi wanaotembelea maonyesho hayo, wamesema wamejifunza mambo mengi na watahakikisha wanapotaka kusoma elimu ya juu, wataweza kuchagua vyuo vyenye sifa na vilivyothibitishwa na taasisi ya elimu ya juu Tanzania.

MWISHO