NA FATMA HAMAD, PMBA
WANANCHI wanaoishi kijiji cha Mjini Kiuyu wilaya ya Wete Pemba, wavunja ukimya na kutoa kilio chao kutokana baada ya kuwekeza nguvu kazi zao na fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya, ingawa kimeshindwa kutumika baada ya kukosa watalamu wa afya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo mwananchi Khamis Omar alisema kuwa walitisha mchango wa fedha, vifaa na nguvu kazi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.
Alisema kuwa kwa wakati huo kila nyumba ilitoa gharama kwa ajili ya ujenzi wa kiyuo hicho ingawa hadi sasa hakija tumika kama malengo yao walivyofikiria.
‘’Kuanzia mwaka 2011,ndipo ambapo kituo chetu hichi kilimalizika ujenzi wake ingawa hadi sasa hakitumiki na kimekaa mithili ya gofu,’’alieleza.
Nae Raya Hassan alisema huu ni mwaka wa 12 tokea kujengwa kwa kituo hicho, ambapo kilifunguliwa kwa mbio za mwenge,ingawa hadi sasa hakija tumika.
‘’Baada ya kuona tunapata tabu kwa kufuata huduma za afya masafa marefu, ndipo tukamua kujitolea kujenga ili tuondokane na shida hiyo,’’alieleza.
Kwa upande Bikame Bakar Darusi alisema mtoto wake alijifungulia njiani wakati wanafuata huduma za uzazi kituo cha afya kilichopo Vitongoji.
‘’Tulitarajia kuwa fedha tulizozitoa, nguvu kazi na michango mengine juu ya ujenzi wa kituo hichi cha afya shida kama hii isingali tufika kama pengekuwa na watalamu,’’alifafanua.
Mapema Diwani wa wadi hiyo Nassra Salum Mohamed alisema tayari wameshafuatilia kila sehemu ili kuona kituo hicho kinatoa huduma, lakini imeshindikana.
‘’Ijapokuwa kinajengwa kituo katika eneo la kiuyu Minungwini, lakini ni vvyema kuwangaliwe tena kwa jicho la pili, kwa vile kijiji cha mjini kiuyu ni kijiji cha ndani, na hakuna hata miundombinu ya barabara,’’ alieleza.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilal Ali alifahamisha kuwa,kwa sasa hawana mpango wa kupeleka watalamu wa afya katika eneo hilo, kutokana na kuimarishwa kwa kutuo cha afya cha Kiuyu minungwini.
Alisema kuwa kwa sasa jengo hilo linatumika kwa shughuli malumu kama vile mripuko wa maradhi pamoja na kipindi cha utoaji wa chanjo za watoto.
MWISHO.