Thursday, November 14

Wizara ya Elimu itaendelea kushirikiana na wadau wa Elimu

ABDI SULEIMAN,PEMBA

WIZARA ya Elimu na mafunzo ya amali imesema kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali wa Elimu ikiwemo Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation katika kupeleka mbele maendeleo ya Elimu nchini.

Hayo yalielezwa na Mratibu Utumishi na Uendeshaji wa Wizara ya Elimu Pemba Maalim Harith Bakar Waziri huko katika kituo cha  ubunifu wa Kisayansi (HUB) huko Pujini Wilaya ya Chake Chake katika siku ya kuazimisha siku ya kusoma na kuandika Duniani.

Alisema taasisi ya Milele Zanzibar Foundation imekuwa ndau mkubwa wa kusaidiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika suala zima la Elimu kwa wananchi wake.

Alieleza kuwa siku ya kusoma na kuandika ni muhimu sana na ndio shirika Umoja wa Mataifa kuitangaza siku ya tarehe 8/9 ya kila mwaka kuwa ni siku ya maadhimisho hayo.

Mratibu huyo aliwataka walimu kuzidisha bidii katika kuwaelimisha Wanafunzi masomo mbali mbali kwani licha ya juhudi kubwa wanazo zichukuwa lakini bado kuna mapungufu kwa Wanafunzi wao hususan katika kujibu majibu ya somo la hesabu.

“ Nichukuwe fursa hii kuipongeza Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa ushirikiano wao mkubwa katika kufanikisha maazimisho haya sambamba na kuandaa mashindano ya kujibu masuala ya masomo mbali mbali kwa Wanafunzi ambayo yametupa fursa  kuona uwezo wa Wanafunzi wetu”, alisema.

Alieleza kuwa ni vyema kwa Walimu kuongeza mbinu za ufundishaji , kwa vile wamekuwa wakipatiwa mafunzo mbali mbali yakumfanya mwanafunzi aweze kufahamu vyema.

Maalim Harith aliwataka walimu wakuu kuendelea kusimamia walimu wao katika kuhakikisha wanafanyakazi kwa weledi ili mapungufu madogo madogo yaliopo kwa wanafunzi katika kujibu masuala yanapatiwa ufumbuzi .

“ Nivizuri Walimu wanapofundisha kuwapatia vitabu wanafunzi ili wawe na uelewa nzuri kwani vimeletwa kwa ajili ya kujifunzia sio kubakia maofisini”, alisema.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Pemba Mmanga Hamad Mmanga aliwahimiza Walimu kuvitumia vituo vya ubunifu wa Kisayansi  (HUB) kwa malengo yaliokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuwafunza wanafunzi masomo mbali mbali ambayo yatawasaidia katika harakati za kutafuta Elimu.

Aidha alisema ni jambo la busara kwa walimu kuendeleza mpango huo wa kuwashindanisha Wanafunzi wa Skuli mbali mbali kujibu masuala kwani hiyo itawajenga vizuri kielimu .

“ Walimu vitumieni vituo hivi kwa malengo mahsusi kwani ndani yake munavifaa mbali mbali ambavyo mukivitumia vitawasaidia wanafunzi wetu kupata uelewa wa mambo mengi ya kimasomo”, alisema.

Akitowa salamu za Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Ofisa miradi ya Elimu kutoka taasisi hiyo Aisha Juma , alisema wamefarajika kuona wanapewa ushirikiano mkubwa na Wizara ya Elimu pale wanapokuwa na shuhuli ya kuendeleza suala la Elimu na kusema kwamba kunahaja ya kuendelezwa mashindano kama hayo kwani kuna tatizo kubwa la wanafunzi katika masomo ya Sayansi.

Alieleza kuwa kumekuwa na mapungufu makubwa kwa Wanafunzi katika kuandika , kusoma na kuandika na ndio shirika la Umoja wa Mataifa ikaitenga siku hiyo maalumu.

Ofisa huyo aliwasihi Walimu kuendelea na juhudi zao za kufundisha wanafunzi wao kwa bidii kubwa ili waondokane na tatizo hilo kwani wanaouwezo mkubwa wa kufanya hivyo.

Hata hivyo kwa upande wa Mratibu wa kituo cha Ubunifu wa Kisayansi (HUB) Pujini, Moh’d Ramadhan Soud alisema elimu ni jambo muhimu katika maisha ya mwanaadamu kwani bila ya Elimu hakuna kinachoenda , watakitumia kituo hicho kwa kuwaendeleza wanafunzi kielimu ili wafanye vyema katika masomo yao.

    MWISHO.