Monday, November 25

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amewataka wazazi na walezi kuwasimamia vyema watoto wao katika kuwapatia elimu iliyo bora.

Wazazi na walezi wametakiwa kuwasimamia vyema watoto wao katika kuwapatia elimu iliyo bora itakayowasaidia katika maisha yao ya sasa na baadae.

Akiwasalimia Waumini wa Masjid Kheir iliyoko Nyamanzi wakati wa Ibada ya Sala ya Ijumaa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amesema ili watoto wafikie lengo la kutafuta elimu jitihada za wazazi zinahitajika ikiwemo kuwafuatilia na kujua mienendo ya watoto hao.
Alhajj Hemed ameeleza kuwa Serikali inachukua jitihada mbali mbali katika kuimarisha sekta ya Elimu nchini hivyo, ushirikiano wa wazazi utasaidia kwa kiasi kikubwa watoto kupata elimu kwa urahisi.
Ameeleza kuwa Taifa linahitaji wasomi waliobobea katika fani mbali mbali, wenye nidhamu na Maadili mema ambao watasaidia kutoa mawazo ya kuliletea Taifa maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema elimu bora inapelekea kupunguza mmong’onyoko wa maadili, vitendo viovu na kusaidia kurejesha hadhi ya Zanzibar iliyosifika kwa Maadili mema.
Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza wananchi kuendelea kulinda Amani na utulivu iliyopo nchini hatua ambayo itasaidia kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Aidha ameeleza kuwa Msingi wa maendeleo ya Nchi yoyote ni Amani na utulivu hivyo, ni wajibu wa kila mwananchi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna atakaejaribu kuvuruga Amani iliyopo nchini.
Akitoa Khutba ya Sala ya Ijumaa Shekh Hafidh Ramadhan Simai amewakumbusha waumini kumcha Allah (S.W) katika maisha ya kila siku kwa kufanya yote yanayomridhisha Allah na kuacha makatazo yake.
Amesema maisha ya Dunia ni ya kupita hivyo, ni wajibu wa kila Mwanadamu kuzitafuta radhi za Allah kwa kufanya amali njema ili kujiandaa na maisha ya kudumu ya akhera.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
08 Septemba, 2023