NA ABDI SULEIMAN,PEMBA.
KUKAMILIKA kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa nane ya kusomea kwa skuli ya kisasa ya sekondari Chokocho, kutaondosha changamoto ya uhaba wa madarasa ya kusomea na kuingia mikondo miwili kwa wanafunzi wa skuli ya Maandalizi, msingi na Sekondari Chokocho.
Hayo yameelezwa na mwalimu mkuu wa skuli hiyo Haji Soka Khamis, katika hafla ya kupokea vifaa mbali mbali vya ujenzi kwa skuli kutoka kwa mbunge wa jimbo la Mkoani Profesa Makame Mbarawa.
Alisema kwa sasa skuli iliyopo ina inatumiwa na wanafunzi wa maandalizi, msingi na sekondari, jambo ambalo halitoi ufanisi mzuri wakati wa ufundishaji.
“Wanafunzi wanaposoma wanahitaji utulivu wa hali ya juu, sisi sekondari tupo 284 madarasa yaliopo nane unazani hapo uhalisia wa kufundisha utapatikana, hujawaingia wanafunzi wa maandalizi na msingi”alisema.
Aidha alisema kujengwa skuli nyengine itapunguza mchanganyiko wanafunzi, kwani sekondari na msingi zitagawika na wanafunzi kusoma sehemu zao kwa utulivu zaidi.
Hata hivyo alisema skuli hiyo inayojengwa itakua na madarasa nane ya kusomea, ofisi ya mwalimu mkuu, chumba cha kompyuta, vyoo, maktaba na lebrari ambayo itakua mkombozi mkubwa kwao, huku akiwataka wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kusaidia sekta ya elimu ambayo ndio sehemu muhimu kuwekeza kwa watoto.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya sekondari Chokocho Iddi Abdalla Iddi, alisema kujengwa kwa skuli mpya itawafanya wanafunzi madarani kubakia 45, hali itakayopelekea kuongeza kwa ufaulu wa wanafunzi skuli hapo.
“Leo hapa tumekabidhiwa mchanga, safuji, matufali, mawe, kokoto na nondo, kila mmoja wetu ameshuhudia makabidhiano haya kilichobaki ni sisi kuwapatia ushirikiano wajenzi ili jengo letu likamilike kwa wakati,”alisema.
Mapema akikabidhi vifaa vya ujenzi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mkoani Profesa Makame Mbarawa Mnyaa, katibu wa Mbunge huyo Mariyam Said Khamis, aliwashukuru viongozi wa kitaifa wa Tanzania na Zanzibar, kwa kuhakikisha maendeleo yamepatikana nchini, ikiwemo sekta ya elimu, Hospitali za kisasa, masoko ya kisasa na kuwataka wananchi kuwa na imani na viongozi hao.
“Sisi kufika hapa ni wao na kuhakikisha tunaleta maendeleo ya jimbo la mkoani, leo tumekuja kukabizi vifaa vya ujenzi wa skuli ya kisasa, ikiwa ni ahadi ya mbunge wa Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumza na wananchi wa shehia ya chokocho,”alisema.
Aidha alivitaja vitu vilivyokabidhiwa kwa hatua ya awali Matufali 8000, sariji mifuko 300, nondo 120, mawe gari 30, mchanga gari 10, kokoto gari tano, ambappo ujenzi huo kwa hatua ya kwanza utagharimu Shilingi Milioni 50.
“Tulianza na Mkanyageni kujenga skuli, Shidi, Michenzani, Ngombeni na sasa ni zamu ya Chokocho, tunakumbuka mwalimu mkuu ulisema unahitaji vyumba vinne vya kusomea sasa kutajengwa vyumba vinane vya kisasa,”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana na mafundi wa ujenzi, pamoja na kulinda vifaa vitakavyotumiwa katika ujenzi wa skuli hiyo, kwani maendeleo ya shehia ya chokocho vhayatolewa na wananchi wengine bali ni wanachokocho wenyewe.
Kwa upande Mwengine Mbunge huyo alimtaka mjenzi wa skuli hiyo, kuhakikisha anawatumia vijana wa shehia husika katika ujenzi huo kwa kuwapatia ajira vijana hao, ili kuondokana na tabia ya kukaa maskani na kufanya mambo yasio faa.
Nae katibu wa UWT Wilaya ya Mkoani Amina Haji Khamis, alisema mbunge wa jimbo hilo ni mzalendo na lengo lake ni kukuza elimu katika jimbo na kutoa viongozi watakao saidia jimbno hilo.
Aidha aliwataka wazazi kutambua kua wanawajibu mkubwa wa kuhamaisha watoto wao katika suala la elimu, kwa kushirikiana na walimu ili kuweza kupata wataalamu wa baadae.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa jimbo la Mkoani Omar Ngwali, aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuendelea kushirikiana na viongozi wao wa jimbo na serikali katika kusaidia huduma za kijamii.
Mbunge huyo pia alikagua ujenzi wa Tawi la CCM milimuni Chokocho ujenzi wake unaoendelea.
MWISHO