Thursday, January 9

Wanamtandao wa kupinga udhalilishaji wa kijinsia kisiwani Pemba wawasilisha  ripoti  ya utendaji kazi zao

NA AMINA AHMED – PEMBA.
CHAMA cha cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar Tamwa kimezipongeza mtandao wa kupinga udhalilishaji wa kijinsia kisiwani Pemba kwa kuendelea kusaidia jamii kuripoti matukio hayo yanapojitokeza katika maeneo yao ambapo wamewaasa wanamtandao hao kuendelea na harakati hizo ili kusaidia Serikali Kumaliza vitendo vya Udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Akizungumza na watendaji wa Mtandao huo wilaya ya Mkoani Wete na Micheweni kisiwani Pemba katika kikao maalum cha uwasilishaji ripoti ya utendaji wa kamati hizo, Afisa mradi wa tumia jukwaa la habari kumaliza vitendo vya udhalilishaji kutoka @tamwa_zanzibar Zaina Abdalla Salum amesema mafanikio ya kupambana na vitendo hivyo kisiwani Pemba yametokana na uelewa uliojengeka kupitia wanamtandao hao jambo ambalo limesaidia kuchukuliwa hatua kwa kesi mbali mbali za Udhalilishaji zilizojitokeza katika mwaka 2021,2022 na 2023.
Nae Afisa ufuatiliaji na Tathmini kutoka @tamwa_zanzibar Abdulrahman Muhamed Abdulahman amewataka wanamtandao hao kuendeleza mashirikiano na chama hicho katika harakati za kupambana na Udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya kujikinga kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria juu ya vitendo hivyo vinapojitokeza.
Kwa Upande wake Mratibu wa Chama hicho kisiwani Pemba Fat-hiya Mussa Said amesema licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali wanamtandao hao wamekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia jamii kuripoti kesi za udhalilishaji zinapojitokeza .
Wakizungumza baadhi ya wanamtandao hao akiwemo Awena Salum Kombo, Bakari Khamis Shehan pamoja na Haji Shoka wamesema mradi huo wa kutumia jikwaa la habari kumaliza vitendo vya udhalilishaji umekuwa chachu ya kuleta mabadiliko katika kesi mbali mbali zilizoripotiwa ikiwemo kupatiwa hukumu stahiki.
Aidha wanamtandao hao wameomba uongozi wa @tamwa_zanzibar kuendelea kupambana na changamoto mbali mbali zilipo katika jamii ambazo zinarudisha nyuma mapambano dhidi ya udhalilishaji ikiwa ni pamoja na Rushwa muhali, jamii kukosa imani, sheria zisizotekelezeka, Pamoja na watoto wanaokinzana na Sheria.
Kikao hicho cha uwasilishaji ripoti  ya utendaji  kwa wanamtandao hao kimefanyika katika ukumbi wa Tamwa  Mkanjuni Chake Chake Pemba  mapema leo asubhi ambapo  ripoti dhidi ya ufuatailiaji wa kesi za udhalilishji, ulawiti utekelezwaji wa watoto,  kesi zilizotolewa hukumu na  shambulio la aibu zimewasilishwa katika ripoti hizo.
MWISHO.