Saturday, March 15

Sylvestre Ilunga Ilukamba atakiwa kujiuzulu ndani ya saa 24

Wabunge nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamepiga kura kumuondoa madarakani Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga Ilukamba

Bwana Ilukamba, ambaye hakuwepo wakati wa kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa bungeni, amepewa saa 24 kujiuzulu.

Wabunge wanamshutumu Bw. Ilukamba, mshirika wa rais wa zamani Joseph Kabila, na mawaziri wake kwa utendaji kazi mbovu.

Kuanguka kwa serikali kunafungua milango kwa Rais Félix Tshisekedi kuteua mawaziri watiifu kwake.

Mweezi uliopita, Rais Tshisekedi aliuvunja muungano ulioundwa na mtangulizi wake, umoja ambao mawaziri washirika wake walitawala kwenye baraza la mawaziri.

Tangu wakati huo, Bw. Tshisekedi amekuwa akiwashawishi wabunge kuachana na muungano wa Bw Kabila, ambao hapo awali ulishikilia wengi bungeni, ukikwamisha mpango wa rais wa mageuzi.

Hii itakuwa ni kwa mara ya kwanza nchini DRC katika historia ya miaka 60, serikali ikilazimishwa kujiuzulu.

Mpango wa kuvunja muungano.

Rais wa Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, aliamua kuweka mpango wa kuvunja serikali ya muungano na wafuasi wa aliyekuwa rais wa taifa hilo, Joseph Kabila.

Felix Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila waamua kuunda serikali ya muungano

CHANZO CHA PICHA,TONY KARUMBA

Amesema alipata ushauri wa wiki tatu kabla ya kutoa tangazo hilo la kusitisha serikali ya muungano.

Bwana Tshisekedi alisema alishindwa kutekeleza mahitaji ya Wakongo kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na changamoto hiyo.

Hivyo jambo muhimu ambalo ameliafikia ni kuchagua maafisa wapya kuunda baraza jipya kwani bunge la sasa lina wafuasi wengi wa Kabila ambao hawamsikilizi.

Alisema alikuwa amejiandaa kuvunja bunge lote kama kuna ulazima.

“Ni wakati muafaka wa kuzingatia maadili, kanuni na mfumo wa mipango iliyopo.Hivyo ni muhimu kufanya mageuzi yakinifu na sahihi katika bunge lililopo sasa ni muhimu”.Alisema Rais Tshiskekedi.

”Kwasababu hiyo, nimeamua kumteua ‘mtoa taarifa’ ,kwa mujibu wa katiba kifungu namba 78, aya ya pili.” aliongeza

Mtoa taarifa huyo atawajibika kuainisha watu watakaokuwepo kwenye serikali mpya ya muungano, ambayo itakuwa na wajumbe wengi ambao ni wafuasi wa chama kilichopo madarakani tofauti na awali.

Kwa mujbu wa Rais Tshisekedi, utakuwa muungano mpya ambao serikali utauweka na kufanya kazi kwa miaka iliyosalia ya uongozi wake.

Kwa maono yake ili kufanikisha kukidhi matakwa ya watu mabadiliko hayo yanapaswa kufanyika.

Kwa maana nyingine , sababu ya kusitisha muungano huu ni kukabiliana na mvutano uliopo ambao unaweka kizuizi katika jitihada za serikali.

Takribani miaka miwili sasa, DRC iliunda serikali ya muungano , baina ya chama cha kabila na chama cha rais mpya Tshisekedi, vyama viwili ambavyo vilipingana kwa kipindi cha muda mrefu vilikubaliana kufanya kazi kwa pamoja, lakini baada ya siku chache tu mvutano ulianza kati ya vyama hivyo.

Baadhi ya wafuasi wa chama cha Tshisekedi walianza kususia ushirikino huu, huku wakiwashutumu wafuasi wa chama cha Kabila kumzuia rais mpya kutekeleza ahadi zake.

Serikali ya DRC, ina mawaziri 60 ambapo 42 wanatoka katika chama cha Kabila huku 23 wakitoka katika muungano wa bwana Tshisekedi.