Sunday, November 24

Wakulima mboga mboga wakutanishwa na wafanyabiashara

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

WAKULIMA wa mazao ya mboga mboga, wafanya biashara na wadau wengine kisiwani Pemba, wametakiwa kuwa na mahusiano ya karibu ili waweze kushirikiana katika kutatua changamoto inazowakabili.

Wito huo umetolewa na Mtafiti na Mtaalamu wa Kilimo Biashara kutoka shirika la Kimataifa la utafiti na uendeshaji wa mazao mboga mboga, matunda na viungo (World Vegetable Center) Judith Assenga, wakati alipokua akifungua warsha ya kuwaunganisha wakulima wa mboga mboga na wadau mbali mbali na kufanyika mjini Chake Chake.

Alisema endapo wakaungana kwa pamoja wataweza kutatua, changamoto nyingi na kufikia mahali changamoto ya soko, kifedha zitaondoka kwa wakulima na wafanyabiashara kunyanyuka.

Aidha alisema lengo kuu ni kuwawezesha kujenga mahusiano ya karibu, kwani tatizo kubwa ni kuuza mazazo yao kwa bei ndogo na kutokujua tatizo la soko liko hali gani.

“Munganiko wao na uhusiano ya karibu, utapelekea wakulima kujua mazo gani wanatakia kulima na soko lake, kwani lazima sasa washirikiane na wafanyabiashara kabla ya kuzalisha mazao,”alisema.

Aidha alisema tatizo kubwa linalowakumba wakulima ni kuuza mazo yao kwa bei ndogo, kutokana na kutokujua taarifa za masoko, na kutokua na mahusiano na wafanyabiashara hali inayopeleka wakulima wengi kupata hasara.

“Tunaamini kuanza sasa mkulima hawawezi kupata tena changamoto wakati wa kuuza mazao yake, kulanguliwa mashambani na wale wanao waita madalali, tayari tumeshawajengea mahusiano mazuri katika shuhuli zao za kilimo,”alisema.

Hata hivyo aliwataka hao kulima na mazao tofauti na sio kujikita na zao moja tu, jambo ambalo linapeleka kukosekana kwa faida na kusababisha bei kushuka.

Kwa upande wake Afisa wa maendeleo ya kilimo wilaya ya Chake Chake Rashid Mohd, alisema changamoto zinazowakabili wakulima ni kutokuangalia mbegu bora inayopendwa na wafanyabiashara na zao linakaa muda mrefu bila ya kuharibika.

Aidha alisema wakulima wanapaswa kuangali suala zima la ubora wa bidhaa zao, na kuzibagua kwa kuangali bei kwa mujibu wa bidhaa wakati wa mauzo.

Akitolea mfano afisa huyo, alisema mbegu za tungule wakulima walio wengi hawana kawaida ya kuangalia mbegu bora, na zinazokaa muda mrefu bila ya kuharibika, jambo ambalo hupelekea hasara na kuoza kwa bidhaa hizo.

“Kabla ya kulima angalieni na soko linahitaji bidhaa gani, sio sote tunapanda tungule tena kwa muda mmoja, hapo hatutofanya vizuri lazima bidhaa zitakuja kwa wingi sokoni na bei kushuka, “alisema.

Hata hivyo aliwataka wakulima hao kwenda kupima udongo wa shamba, wanalotaka kulima kabla ya kuanza kulima ili kujua ni aina ngani ya mbegu itakuwa na mbolea.

Nae Kaimu Mratibu mitaji na mikopo (ZEEA) kutoka ofisi ya kazi uchumi na uwekezaji Pemba Haji Khamis Haji, alisema Serekali ina njema ya kuwasaidia wananchi wake, ndio maana ikawapatia mikopo ili iwasaidie kwenye shughuli zao.

Hata hivyo aliwataka wakulima kuichangamkia fursa zinazotolewa na idara hiyi, ili kuweza kuongeza thamani ya bidhaa kwa wakulima.

Aidha Afisa huyo alizitaja fursa za mikopo ya Covid 19, alisema vijana wana 45%, wanawake 35%, wastaafu 12%, watu wenye ulemavu 5% na waliobadili tabia (walioacha kutumia dawa za kulevya 3%).

“Serekali imetaka jamii kuanzisha vikundi vya ushirika, ili iwe rahisi kupatiwa mikopo hiyo haitolewi kwa mtu mmoja mmoja, bali hutolewa kwa vikundi kama ni wanawake wawe ni wanawake watupu, kama ni vijana wawe ni vijana tu, ikiwa ni wanaume au wanawake na wanawake cha msingi wawe ni vijana, kama ni walemavu wawe peke yao,”alisema.

Nae mtoa huduma za Pembejeo za kilimo Wilaya ya Chake Chake,  kutoka kampuni ya Agrodilar Altaqwa Sultan Said Suleiman, alisema vitu vinavyosababisha kuharibika kwa mbegu ni wakulima kukosa mbinu ya kujua ubora wambegu husika na mbolea inayoendana na udongo wa eneo.

“Mfano mkulima ataweka mbolea wakati tungule, imeshazaliwa hali hiyo inaweza kusababisha tungule kupasuka na kuzifanya ziharibike,”alisema.

Nae Rahma Mabrouk Heri kutoka kikundi cha Marwa, kinachojishuhulisha na usanifu mazo kutoka Wawi alisema changamoto kubwa nayowakumba katika kikundi chao ni upatikanaji wa malighafi, vifaa vya usindikaji kama blenda, changamoto za usajili ZBS na ZFDA pamoja na vifungashio.

Aidha aliyomba serekali, sekta binafsi kuweka duka la vifungasho na malighafi kisiwani hapa, litakalouza kwa bei nafuu na itakayowasaidia kuuza na kupata faida.

“Endapo tutawekewa duka hapana kisiwani Pemba ile gharama ya kutumia kwenda kuvitafuta itapungua na ukiangalia sisi bado ni wajasiriamali wachanga tunahitaji kukuza ujasiriamali wetu na soko” Amesema Rahma.

Nae mkulima Said Yussuf Ali kutoka kikundi cha Juhudi endelevu, alisema kukosa soko la uhakika kwa ajili ya bidhaa zao, sehemu ya kuhifadhia mazao na ushukaji wa bei kiholela, ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakumba wakulima walio wengi.

Jumla ya vikundi 20 vimeshafikiwa kwa upande wa Pemba, ambavyo vyote ni kutoka Wilaya ya Chake Chake na Shirika la kimataifa la utafiti na uendeshaji wa mazao mboga mboga na matunda (world Vegetable Center) kwa ufadhili wa USAID, IFRDC na CIMMYT chini ya mradi wa uharakishaji na uendeshaji wa Teknolojia.

MWISHO.