Wednesday, January 15

RC MJINI MAGHARIBI:APRM NI JUKWAA ZURI LA KUCHAKATA FIKRA ZA MAENDELEO NA TANZANIA KUPAA KIUTAWALA BORA DUNIANI

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mheshimiwa Idrissa Kitwana Mustafa amesema kuwa APRM Tanzania ni jukwaa zuri ambalo linamgusa kila mdau Tanzania, hivyo amewataka watendaji wa APRM kuhakikisha kuwa taarifa wanazozitoa wanazichakata vizuri ziweze kuleta maendeleo na kuifanya Tanzania iweze kupaa katika masuala ya Kiutawala Bora duniani.

Rai hiyo ameitoa mapema leo hii, wakati alipokutana na uongozi wa APRM Tanzania walipofika Ofisini kwake Vuga kwa lengo la kujitambulisha na kuelezea mikakati mbalimbali kuelekea Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora Tanzania.

Mheshimiwa Kitwana amesema kuwa umuhimu wa APRM ni mkubwa mno kwa Serikali lakini pia kwa wananchi kwavile ni chombo rasmi cha Serikali ambacho kinafanya tathmini kwa kuchukua maoni moja kwa moja kwa wananchi kwa lengo la kuimarisha masuala mbali mbali nchini, hivyo wataalam wanaokusanya maoni hayo wanapaswa kuwa wazalendo ili kuhakikisha kuwa Ripoti zinazoandaliwa zinakuwa na ubora kulingana na hali halisi ya Tanzania ilivyo.

Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa, APRM Tanzania inapaswa kushuka chini zaidi kwa wananchi katika ngazi mbali mbali ikiwemo za Wilaya, Wadi na Shehia kwa lengo la kuwafahamisha wananchi umuhimu wa chombo hicho na ushiriki wao katika maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora.

Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Lamau Mpolo amesema kuwa APRM inajipanga kuhamasisha umma kuhusu maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora hivyo imepanga kupita kwa viongozi wa Kitaifa Chama na Serikali kwa lengo la kupata ridhaa, miongozo na Baraka zao na hatimae itafika kwa wananchi kwa ngazi mbali mbali kukusanya maoni ambayo yatatumika katika Ripoti hiyo ya Tathmini.

Katibu Mtendaji Lamau ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi mazuri na makubwa mabayo yanahitajika kuwekwa kimaandishi kama ni Ripoti rasmi ya nchi na pia dunia iweze kutambua mazuri hayo yanayohusu Utawala Bora Tanzania, hivyo ameomba mashirikiano kwa kila mdau katika kulifanikisha hilo.

Vile vile uongozi wa APRM Tanzania ulipata fursa ya kuonana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini Unguja Ndg Radhia Rashid Haroub ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mhe Hadid Rashid Hadid amesema kuwa Uongozi wa Mkoa wa Kusini upo tayari muda wowote kufanya kazi na APRM Tanzania kwavile unafahamu umuhimu wa Ripoti hiyo ni kwa maslahi ya Nchi.

Ameongeza kuwa APRM Tanzania inapaswa kuongeza nguvu zaidi katika suala la kutoa elimu kuhusu APRM na maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ili wananchi waweze kuifahamu vizuri zaidi na waweze kutoa maoni yao kwa undani katika kuitathmini Serikali yao.