Wednesday, January 15

Wadau wa Sheria wajadili na  kutoa Maoni  katika  rasimu ya sheria ya kuanzishwa mahakama maalum  ya rushwa  na uhujumu uchumi.

NA AMINA AHMED-PEMBA.

WADAU wa sheria kutoka Taassisi mbali mbali za Serikali pamoja na taasisi binafsi  kisiwani Pemba  wameshiriki katika  mkutano maalumu wa kujadili na  kutoa Maoni  katika  rasimu ya sheria ya kuanzishwa mahakama maalum  ya rushwa  na uhujumu uchumi   uliondaliwa na  ofisi ya mwanasheria mkuu Zanzibar   wenye lengo la kuboresha na  kupatikana kwa sheria  bora  itakayosimamia masuala hayo.

 

Wakitoa maoni yao mara baada ya kufanyiwa mapitio ya rasimu hiyo  baadhi ya wadau hao  akiwemo Muhammed  Ali  Muhammed   kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka,  Simba Khamis Simba  kutoka  kikosi cha kuzuia magendo Zanzibar   (KMKM)  wameiomba kamati  inayosimamia   rasimu hiyo kuongeza Vifungu vya sheria  ambavyo vitaweza kusimamia suala la usafirishaji haram wa magendo ya karafuu, mazao ya baharini pamoja na  usafiriahaji haramu wa binaadamu.

 

Wamesema  miongoni mwa mapungufu ambayo yamejitokeza katika rasimu ya sheria hiyo ni kukosekana kwa vifungu vinavyoonesha  masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi katika  zao la karafuu na mazao mengine  ya baharini  pamoja na Usafirishaji wa binaadamu  ambapo  kuingizwa  vipengele hivyo kutasaidia  kuisaidia serikali ya Zanzibar kutimiza azma yake kukuza na kuimarisha zaidi sekta ya uchumi  wa buluu  pamoja na biashara.

 

Aidha kwa upande wao   Asya Issa Hemed , Neema  Juma   pamoja na Seif Muhammed Khamis   hakimu mahakama ya mkoa  Kaskazini   hakimu mahakama wilaya pamoja na   Wakili wa Seriki kutoka  ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka Wameiomba  kamati hiyo kuondoa vipengele   vilivyoweka ukomo wa kusikilizwa kesi  na badala yake kutoweka ukomo huo kuongeza  faini kubwa isiyopungua Milioni 100 badala ya milioni 50.

 

Awali akizungumza na wadau hao kaimu Mrajisi wa Mahakama Kuu Pemba Faraji Shomari Juma amesema lengo la kuwakutanisha wadau hao wa masuala ya kisheria kutoka taassisi mbali mbali ni kuongeza maboresho kwa kupata mawazo bora zaidi katika  kuimarisha rasimu hiyo ambayo yatasaidia kupatikana kwa sheria bora itakayoweza kusimamia masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi.

 

Akizungumza mara baada ya kutolewa maoni hayo katibu wa kamati maalumu  ya kukusanya maoni   juu ya sheria ya  kuanzishwa  mahakama maalum ya kuzuia Rushwa na Uhujumu wa uchumi Zanzibar Said Salum Said  ambae pia ni wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu Zanzibar ameahidi kuyafikisha  maoni hayo  yaliyotolewa na wadau hao ili kuweza  kufanyiwa kazi.

 

Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa baraza la mji Chake Chake umejumuisha wadau wa sheria  kutoka Taasisi mbali mbali ikiwemo  Mamlaka ya kuzuia Rushwa na uhujumu uchumi, Jeshi la Polisi  mahakimu wa mahakama za Wilaya na Mkoa , Mawakili wa kujitegemea kutoka taasisi za serikali na binafsi,   waendesha Mashtaka wa Serikali, Waasheria  wa Serikali, wadau kutoka mamlaka  ya kudhibiti dawa za kulevya, pamoja na  KMKM, ambapo  Kujadiliwa kwa  rasimu  hiyo ya kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kupambana na rushwa  na uhujumu uchumi Zanzibar  ni utekelezaji wa agizo la  rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi alilolitoa Siku ya sheria juu ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo maalumu.