Wednesday, January 15

Uzinduzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar

Wazee wakiwa katika vazi rasmini la Utamaduni wa Zanzibar Baibui la Ukaya na Kanga za Kisutu wakisuka ukiwa wakati wa Ufunguzi wa Tamasha la Utamaduni wa Mzanzibar linalofanyika katika viwanja vya Mao Zedung Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar, kwa maonesho mbalimbali.

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema uhuru wa utamaduni ni muhimu katika kujenga na kudumisha hali za uvumilivu na heshima kwa jamii.

Tabia aliyasema hayo wakati akizindua tamasha la 28 la utamaduni wa Mzanzibari katika viwanja vya Mao Zedong mjini Unguja.

Alisema ni vyema kuhakikisha tamaduni zinatumika katika kusaidia pamoja na kuziunganisha jamii mbali mbali za ndani na nje .

Alieleza kwamba baadhi ya watetezi wa uhuru wa kiutamaduni wanalenga na kutetea kufuatwa kwa maadili yasiofungamana vyema na mila ambazo wakati mwengine mambo hayo huvunja sheria za kimaadili na hata sheria za nchi zilizopo.

Aliwataka wasanii kuwa na tahadhari kubwa katika kuandaa filamu zao kutokana na wao kuwa ni kioo cha jamii.

Tabia alisema kuimarisha maendeleo ya watu na tofauti za kiutamaduni ni changamoto kubwa katika Bara la Afrika na dunia nzima.

Alisema katika mazingira ya sasa mambo manne muhimu yanahitahika katika kufanikisha lengo hilo .
Aliyataja mambo hayo ni pamoja na kuandaa dira ya maendeleo ya utamaduni, wataalamu wanapaswa kubainisha dira itakayoimarisha shughuli za kiutamaduni,kufanyika tafiti mbali mbali zinazohusiana na utamaduni na kuandaa mpango maalum wa kufuatilia tamaduni za kijamii kulingana na makundi na makundi ya watu waliopo Zanzibar.

kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab alisema kufanyika kwa tamasha hili kutasaidia kuinua na kuimarisha utamaduni wa nchi hii.

Hivyo aliwataka wananchi wakiwemo wasanii kushirikiana na Serikali katika kufanikisha tamasha hilo linalofanyika kila mwaka.

Katibu huyo alisema tamasha hilo linatarajiwa kutoa burudani mbali mbali katika visiwa vya Unguna na Pemba.

Katibu Mkuu huyo aliishukuru Serikali pamoja na taasisi mbali mbali kwa msaada walioutoa kufabikisha kufanyika kwa tamasha hilo

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Idrissa Kitwana Mustafa aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendeleza tamasha hilo.

Alisema kufanyika kwa tamasha hilo kunaleta fursa kwa vizazi vya sasa kujua mila silka na tamaduni za nchi hii.

Kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ” haki na uhuru wa raia hutegemea maadili ya taifa lenyewe”.