Wednesday, January 15

RC Salama elimu ndio chanzo cha maendeleo.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba salama Mbarouk Khatib, amesema suala la elimu ndio chanzo cha maendeleo katika taifa lolote lile duniani, ndio maana kila nchi inawekeza vijana wake katika suala la elimu.

Alisema baada ya Mapinduzi ya Mwaka 1964, kila awamu ya Rais wamekuwa wakilipa kipaombele suala la elimu nchini, ikiwemo kuimarisha kwa majengo ya kisasa na utoaji wa elimu bure.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati wa matembezi ya wanamichezo mbali mbali kutoka Zanzibar, ikiwa ni shamrashamra za kuelekea kilele cha miaka 59 ya elimu bila ya malipo, huko katika viwanja vya chuo cha mafunzo ya amali Vitongoji Wilaya ya Chake Chake.

Alisema baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar hayati Mzee Karume, aliamua kwa makusudi Zanzibar kuikomboa kielimu, ili kuwafanya wananchi wote wa Zanzibar kupata elimu bora bila ya malipo.

“Kila inapofika 23 Septemba kila mwaka tunaadhimisha elimu bila malipo, hayati Mzee Karume alifanya kuwakomboa wananchi wanyonge wakiwa ni wakulima na wakwezi, waweze kupata elimu ya lazima, historia inaeleza kipindi cha wakoloni wazazi wetu hawakuweza kudiriki kupata elimu,”alisema.

Aidha alisema kipindi hiko waliosoma waliweza kufikia darasa la tatu au la nne, waliofika darasa la nane basi walishikwa mikono na wazazi wao, kutokana na kuwa na uwezo.

Alisema suala la elimu Zanzibar limepewa kipaombele, ili kuhakikisha taifa linazalisha wataalamu wazalendo, watakaoweza kuisaidia nchi yao.

Hata hivyo alisema Serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dk. Hussein Mwinyi, imefanya kazi kubwa katika sekta ya elimu, kwa kujenga skuli za gorofa na zile za chini, zikiwa na madarasa ya kisasa ndani ya mikoa yote mitano ya Zanzibar.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Mkoa, aliwataka wanafunzi kutokuchezea elimu, fursa haiji mara mbili na wakati unakwenda na haurudi, kwani walianza mwaka 1964 sasa mwaka 2023 na tayari maendeleo makubwa yamepatikana chini ya uongozi wa Rais Dk.Mwinyi.

Hata hivyo aliwataka wanafunzi watakapomaliza elimu zao za sekondari kuhakikisha wanajiunga na vyuo vikuu kwa watakaobahatika, waliobakia kujiunga na vyuo vya amali ili kupata fani na ujuzi mbali mbali.

“Sasa si wakati wa kukubali kupotoshwa na mtu yoyote asietaka maendeleo nchini, leo mtoto wa mnyonge anafika chuo kikuu hapa kwetu zipo PHD na masta nyingi sana ushindani wa elimu sasa umekua,”alisema.

Nae Mkuu wa wilaya ya Chakechake Abdallah Rashid Ali amewasisitiza wanafunzi hao kutambua kuwa michezo ni sehemu yao ya masomo, kwani taaluma inahitaji mtu awe mchangamfu na mwenye afya njema.

“Wale wanafunzi wanaofanya vizuri madarasani basi ni wazuri pia hata katika michezo, unaposhiriki michezo unapata kuichangamsha hata akili yako,”alisema.

Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mohammed Nassor Salim, alisema wanafunzi wote wapo katika hali zalama za kiafya, kwani wanashirikiana ipasavyo na wataalamu wa wafya wakiongoza na afisa mdhamini wa wizara husika.

Mapema Mkurugenzi Idara ya Michezo na utamaduni wizara ya elimu Zanzibar Ahmed Abdalla Mussa, alisema wanafunzi wote watahakikisha wanashiriki kikamilifu katika michezo ikizingatiwa mwaka huu tamasha la elimu bila malipo ni la aina yake.

MWISHO