Friday, March 14

TAIFA CUP IWE CHACHU YA KUIBUA VIPAJI-MAWAZIRI

Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita na Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Michezo Tanzania Bara Damas Ndumbaro wamesema Taifa Cup iwe ni chachu ya kuibua vipaji  kwa vijana katika michezo yote shiriki.

Wakizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya michezo kwa Mikoa ya Zanzibar kwa ajili ya Mashindano ya Taifa Cup, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Migombani.

Waziri Tabia alimpongeza Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuendeleza na kuimarisha sekta ya michezo nchini, lakini pia kuweka hamasa ya kununua magoli katika michezo imewapa ari viongozi katika kuwaamsha vijana katika michezo.

Alisema wataendeleza ushirikiano na Wizara ya Utamaduni, Sanaa  na Michezo Tanzania bara katika kutekeleza majukumu yao kwa wakati ili kuzisaidia Serikali zote mbili lengo kupatikana maendeleo.

Nae Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Damas Ndumbaro alisema ni vyema mikoa kutafuta vipaji ngazi ya chini na hatimae watakapofika Taifa kuendelezwa vipaji hivyo bila ya kuviacha vipotee.

Alisema wanakila sababu ya kulinda, kudumisha na kusimamia Muungano na kuhakikisha atafanya kazi  kwa ushirikiano na Waziri Tabia katika kulinda Muungano na kuimarisha michezo nchini.

Hivyo aliwataka Maofisa Michezo Mikoa kuzilea timu na kuibua vipaji ili kuisaidia Tanzania iendelee kimichezo na kupata vijana imara wa kuweka historia.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab alisema Wizara itaendelea kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuibua vipaji kila Mikoa kwa ajili ya kuviendeleza.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini na kutekeleza malengo ambayo yanawaletea mafanikio wananchi.

Kamishna alisema waliokabidhiwa mipira Maofisa wa michezo ikiwemo Mkoa wa kasakazini Pemba, Mkoa wa Kusini Pemba, Mkoa wa Kaskazini Unguja,Mkoa wa Mjini Magharibi ,Pamoja na Mkoa wa Kusini Unguja.

Jumla ya mipira 270 iligawiwa kwa kila mkoa mipira 54 ,ikiwemo mpira wa miguu 18, mpira wa kikapu 18 pamoja na mpira wa wavu 18.