Friday, February 28

Wataka riadha upigiwe jicho kama mpira wa miguu

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

WACHEZAJI wa Mchezo wa Riadha Zanzibar, wamewaomba wadau kujitokeza kudhamini na kutilia nguvu mchezo huo, ili uweze kupata sifa kama ilivyo mchezo wa Mpira wa Miguu.

Hayo yamelewa na wanamichezo mbali mbali, wakati walipokua wakizungumza na waandishi wa habari hizi, mara baada ya kumalizika kwa mbio za riadha na Rilei katika shamrashamra za kilele cha Tamasha la 59 la elimu bila malipo katika viwanja vya Tibirinzi Wilaya ya Chake Chake.

Mmoja ya wanariadha hao Massoud Ibrahim kutoka skuli ya Bumbwini, alisema umefika wa kati mchezo huo kupata udhamini na kuchezwa kila wakati kama ilivyo kwa mpira wa miguu.

“Sisi wanafunzi tunajitahidi kuibua vipaji vyetu, lakini kama hatutapata mfadhili basi tutashindwa kufikia malengo yetu, sisi tusubiri mashindano ya elimu bila malipo kila muda,”alisema.

Aidha aliwataka wanafunzi wenzake kujiingiza katika michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu, Riadha, kwani michezo inajenga mwili, kuboresha kiwango cha elimu na akili inazidi kutanuka.

Nae mwanafunzi Salum Omar kutoka Skuli ya Gando, aliwasihi vijana wenzake kujikita katika michezo kwani michezo afya na ajira kubwa duniani.

Hata hivyo aliwataka wazazi kuendelea kuwashajihisha vijana wao kushiriki katika michezo, kwani michezo hupelekea mwanafunzi kuongeza ufahamu darasani.

“Mategemeo yangu ni kufanya vizuri katika mbio hizi, lakini unavyopanga wewe na mungu anapanga vyake sasa hali haikuwa nzuri kwangu leo,”alisema.

Kwa upande wake mratiba wa Idara ya Michezo na Utamaduni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mzee Ali Abdalla, alisema tamasha la elimu bila malipo mwaka huu, limewafanya wanafunzi kuwa na hamu kubwa ya kujuwa bingwa wa mashindano hayo kwa ujumla mkoa gani, kutokana na ushindani ulivyokuwa mgumu katika michezo.

“Kila skuli mara hii imejipanga kikamilifu, skuli zimekua na ushindani mkubwa kwenye michezo yote, inayofanyika katika tamasha hili,”alisema.

Aidha alisema Wizara kupitia idara ya Michezo na Utamaduni, itaendelea kuibua vipaji vya wachezaji wa riadha maskulini, kwa kushirikiana na chama cha riadha Zanzibar na walimu wa michezo maskulini.

Msaidizi katibu wa Chama cha Riadha Zanzibar upande wa Pemba na mwalimu wa Riadha Farhat Ali Said, alisema mchezo huo umekosa msisimko kama ulivyo mpira wa miguu.

Alisema riadha ni mchezo kama ilivyo michezo mengine, hivyo aliwataka wadau kujitokeza kusaidia vifaa mbali mbali vya michezo kwa ajili ya mchezo huo, pamoja na kufadhili mashindano mbali mbali ya riadha kama ilivyo mpira wa miguu.

MWISHO