Sunday, November 24

Wanawake wajawazito Mwera wanachelewa kuanza Kliniki.

KITUO cha Afya Mwera kilichopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ni miongoni mwa mwa vituo vya afya ya Serikali ambavyo vinatoa huduma za mama na mtoto.

Kituo hicho kilichopo mita 2 kutoka barabara kuu wa lami kinachohudumia zaidi ya wananchi 5000 kwenye huduma za afya bado kinakabiliwa na changamoto ya wanawake wajawazito kuwahi kufika kliniki na kuanza huduma hizo mapema mara tu wanapopata ujauzito.

Akizungumza hali halisi ya wanawake wajawazito katika kituo hicho Muuguzi wa zamu ambaye yupo kwenye kituo cha Afya Mwera Agnes Yohanna amesema wanawake walio wengi wanaokuja kuanza kliniki ni tayari wamefikisha miezi mitatu au minne ya ujauazito wao jambo ambalo si salama kwa afya ya mama na mtoto.

“Kiutaratibu haswa mama anatakiwa kuja kupima na kuona ikiwa amegundulika au umejigundua kuwa ameshakuwa mjamzito aanze kliniki mapema kupata huduma na vipimo na kufuatilia maendeleo yake ila hapa kwa mwezi tunaweza kupokea wajawazito wapya na wanaondelea na kliniki ni wajawazito 250 hadi 300” Agnes Yohanna.

Agnes amesema athari za mama mjamzito kutokuhudhuria kliniki mapema ni pamoja na kutokujua maendeleo yake na mtoto kutokujulikana pia magonjwa ya nyemelezi pamoja na kukosa vipimo vya vya afya yake mapema.

“Wengi wanaficha kwamba jamii isijue ila unapoficha hata wataalamu wa afya basi afya yako ya uzazi inaweza kuwa hatarini hapo mwanzo au hata mwishoni maana maendeleo yako naweza kukuathiri wewe kama mjamzito usijue “Aliendelea kusema.

Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mila na utamaduni wa wanajamii kuficha kutokujuliana kuwa ni wajawazito ni miongoni mwa sababu ambazo zinakwamisha huduma bora za afya ya uzazi kwa wanawake wajawazito.

Leo ni siku ya kliniki na hapa kwenye kituo cha Afya Mwera tayari vibaraza viwili ambavyo vinatazamana vimejaa wanawake ambao wameshika magamba yao tayari kwa ajili ya kupata huduma .Hasina Said Alawi 29,mama wa mtoto mmoja mkaazi wa Mwera hii ni mara yake ya pili kuhudhuria kliniki ujauzito wake kwa sasa una miezi sita maana yake alikuja hapa akiwa na ujauzito wa miezi mitano amesema yeye alishauriwa na dada yake atulie kwanza mpaka miezi sita ndio anze kuja kliniki.

“Mwezi wa tano hivi nikaaza kuumwa na kutokwa na damu ndipo nikaja hapa nikaulizwa gamba la Kliniki nikasema sina nilipopima nikagundulika nilikuwa nafanya kazi nyingi na kunyanyua vitu vizito,kuna faida sana ya kuja hapa mapema maana mimi hii ni mimba yangu ya pili naharibu” Amesema Hasina huku akinyanyuka kwenda chumba cha vipimo kupima shinikizo la damu.

Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amesema Zanzibar bado inakumbana na changamoto ya masuala ya Afya ya uzazi kwa upande wa vifo vya mama kwa mwaka 2021 vifo vya mama kujifungua vilikuwa 130 kwa kina mama 100,000 ambapo ni vingi ukilinganishwa na mpango wa maendeleo endelevu ya kimataifa kuwa vifo 70 kati ya mama 100,000.

Hali ya kuchelewa kufika kliniki kwa wanawake ni jambo linalohitaji elimu ya hali ya juu kwenye jamii jambo pia linaingiliana na suala la mila na utamaduni wa kuamini kuwa kusema au kujionesha mapema kwa mama mjamzito ni kupata kijicho. Zubeda Ali Mfaume, 32 mama wa watoto tatu suala la kuwahi kuja kliniki pale anapogundua kuwa ni mjamzito ni jambo gumu kwake licha ya kuwa na uzoefu amesema kwake huona muda bado upo na hakuna haraka ya kuharakisha kwenye hilo.

“Mimi mara nyingi nakuja mimba nikiwa na miezi mitano maana hapo ndo naanza kuumwa ila kuwahi mapema naona kama najisumbua japo ukija hapa kwa kuchelewa ni suala ambalo madaktari wanatusema ila ndo tushazoea“Amesema Zubeda.

Mkurugenzi Kinga kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Daktari Salim Slim amesema suala ya jamii kuficha ujauzito ni jambo linahatarisha afya ya mama na mtoto na lazima usiri na muhali katika familia uondoshwe katika jamii ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

“Kwa sisi huku Zanzibar mtu akipata mimba unatakiwa ufiche ili kuzuia hasad kwa watu ila familia haitazami suala la afya kwa mama na watoto na ni vyema suala hili liachwe maana litapunguza maafa kwenye kuwalinda kina mama na watoto ambao afya yao ni muhimu sana.” Amemalizia Daktari Salim Salim.