NA OMAR HASSAN – ZANZIBAR
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi MHE, MHANDISI HAMAD YUSSUF MASAUNI amesema kuna haja ya kuwekwa mfumo mzuri wa mashirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi katika kutekeleza sera ya Polisi Jamii ili lengo la kuondoa uhalifu katika jamii lifanikiwe.
Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bububu, katika Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi amesema japo kuwa yapo mafanikio katika usimamizi wa ulinzi na usalama lakini bado zipo changamoto baina ya pande hizo mbili katika utekelezaji wa ulinzi shirikishi mambo ambayo yanahitaji kurekebishwa.
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP. HAMAD KHAMIS HAMAD amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuchukuwa hatua mbalimbali za kutatua changamoto katika utekelezaji ulinzi shirikishi ikiwa pamoja na kujenga uwelewa kwa Askari na wananchi.
Nae Mbunge wa Jimbo la Bububu MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA amewahimiza wananchi kushirikiana na Taasisi za haki Jinai katika kufuatilia kesi zao na kutoa ushahidi ili zipate mafanikio Mahakamani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A Bi SUZAN PETER KUNAMBI amewasihi wananchi kuondoa muhali na kuwacha tabia ya kuzisuluhisha kesi mitaani hasa kesi zinazohusu udhalilishaji wa kijinsia.