Sunday, November 24

SMZ kuimarisha Sekta ya Elimu Kisiwa cha Kojani kwa kuajiri Walimu wazawa.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kukamilika kwa ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Ghorofa Kojani kutasaidia kuboresha sekta ya elimu kisiwani humo kutaondoa changamoto ya uahaba wa madarasa, walimu na vifaa vya kusomea na kusomeshea.

Akikagua jengo hilo linaloendelea kujengwa katika kisiwa cha Kojani Mhe. Hemed amesema katika kuhakikisha Sekta ya Elimu inaimarika katika Kisiwa cha Kojani Serikali itaajiri Walimu wazawa ambao watafundisha kwa ari na upendo ili kutatua changamoto ya uhaba wa Walimu Kisiwani humo.

Amesema kukamilika kwa Skuli hiyo wanafunzi watapata fursa ya kusoma katika mazingira mazuri pamoja na kuwa na vifaa kwa kisasa vitakavyowasadia kupata ujuzi wa masomo wanayopatiwa.

Amewanasihi Wazazi na Walezi katika Kisiwa cha Kojani kuachana na tabia ya kuwakatisha Masomo Wanafunzi wa Kike na kuwazesha badala yake wawahimize katika kusoma ili kupata Wataalamu wa fani mbali mbali ambao watasaidia katika kukiletea maendeleo kisiwa hicho na Zanzibar kwa ujumla.

Aidha Mhe. Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga shilingi Bilioni ishirini kwa ajili ya kuboresha Miundombinu ya Afya na kuwaahidi wananchi wa Kojani kuwa kituo cha Afya kipya kitajengwa na huduma zote stahiki zitapatikana katika Kituo hicho.

Amemalizia kwa kuwataka Wananchi wa Kojani kutoa ushirikiano katika ujenzi huo wa Skuli ya ghorofa na miradi mengine ya maendeleo itakayojengwa katika Kisiwa hicho ili kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuwaletea maendeleo Wananchi wake.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa ameeleza kuwa Jengo la Skuli ya Msingi Kojani litakuwa na huduma mbali mbali na  limezingatia miundombinu ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum ili nao wapate elimu ya lazima.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali imeona umuhimu wa kujenga Skuli hiyo ya ghorofa na tayari kuna mpango wa kujenga Skuli nyengine eneo la Makaani na kutoa elimu ya ufundi hasa uvuvi wa kisasa ili wanafunzi watakapohitimu masomo yao waweze kujiajiri kupitia sekta ya uvuvi.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)