Thursday, January 16

Mkurugenzi TAMWA ZNZ- “Wataalam wa Afya washirikiane na waandishi wa habari jamii ielewe haki ya Afya ya Uzazi”

Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa akifungua mkutano wa wadau wa habari na wataalam wa Afya.

MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ ametoa wito kwa wataalam sekta ya afya, kuendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari katika kutoa taarifa sahihi, kuhusiana na masuala ya afya ya uzazi  ili jamii  iweze kuvunja ukimya, na  taarifa hizo kuwafiikia vijana ili waweze kujikinga na madhara yanayoweza kuwapata kutokana na kukosa elimu ya masuala hayo.

Dkt.  Mzuri aliyasema hayo akifungua mkutano wa wadau wa habari na wataalam wa afya wenye lengo la kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mradi wa utetezi wa masuala ya afya ya uzazi kwa kutumia vyombo vya habari.

Alieleza ili kufikisha elimu sahihi ni lazima kuweka na kuripoti takwimu za masuala haya, ikiwemo vifo vya mama na watoto, mimba za utotoni.

Aidha pia aliongeza kuwa kutoa elimu ya mnyambuliko wa umri wa kubeba mimba pamoja na athari zinazoweza kutokea kulingana na umri husika ni elimu muhimu inayohitajika kutolewa kwa vijana.

mtaalamu wa ufuatiliaji na tahthmini wa TAMWA ZNZ, AbdulRahman Mohammed alifahamisha lengo la TAMWA ZNZ kupitia mradi ni kuongeza uelewa kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala ya haki ya afya ya uzazi  kwa wanawake na wasichana ili kuwasaidia kuepuka na kujikinga  na madhara  mbalimbali yatokanayo na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.

Kwa upande wake, Zaina Mzee afisa msimamaizi wa mradi huo alisema wamewajengea uwezo waandishi wa habari kuifahamu elimu hiyo na kuwasaidia kuandaa vipindi, na habari za uchambuzi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii juu ya mabadiliko ya tabia na afya ya uzazi kwa ujumla.

“Mradi ulianza na utafiti ambao uligundua kuwa waandishi wengi hawana uelewa juu ya masuala ya afya ya uzazi, hivyo tukaandaa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo na sasa wanaripoti vizuri habari hizi na wanaisaidia jamii kupata huduma stahiki,” alifahamisha afisa mradi huyo.

Amina Hussein, Daktari dhamana wilaya ya Kati Unguja alipongeza waandishi wa habari kwa uthubutu wa kuibua changamoto mbalimbali ambazo tayari zimepatiwa ufumbuzi na kuwaomba kuendelea kuielimisha jamii na kutoa taarifa ambazo zinasaidia jamii kuondokana na changamoto.

Alieleza “Nawapongeza waandishi wa habari kwa kazi kubwa walioifanya ya kuibua changamoto, hivi vitu vikizungumzwa ni vizuri watu wakajua, na serikali inapata kuelewa kuna mapungufu gani kwenye jamii na kuwasaidia kutafta namna ya kurekebisha,” alisema Daktari huyo.

Mwandishi wa habari mkongwe Zanzibar, Salim Said aliomba wataalam wa afya kuwa wepesi wa kutoa mashirikiano kwa kutoa taarifa na takwimu pindi zinapotakiwa na waandishi wa habari ili kuwezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Mara nyingi waandishi wanalalamikia upatikanaji wa takwimu, niwaombe wizara ya afya tujitahidi kuwapa ushirikiano waandishi wa habari wanapotaka taarifa kutoka kwenu, kwani takwimu ni ishara nzuri inayoonesha ukubwa ama udogo wa tatizo,”alisema Salim Said.

Mradi wa kuendeleza utetezi wa vyombo vya habari juu masuala ya haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana wa mjini na vijijini ,ni mradi wa mwaka mmoja ambao  unatekelezwa kwa mashiriano na TAMWA ZNZ pamoja na  shirika WELLSPRING.

 

Communications Department,

Tanzania Media Women’s Association- TAMWA Zanzibar,