NA ABDI SULEIMAN,PEMBA
AFISA Tehama Kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Tamima Is-haka Mzee, amewataka wananchi Kisiwani Pemba kuyatumia maonesho ya siku ya Chakula Duniani, yanayoendelea katika viwanja vya Chamanangwe, ili kujifunza mambo mbalimbali hasa taasisi za kiserikali zinazosimamia mapato ya nchi.
Alisema wananchi wanapotembelea taasisi hizo, wataweza kufahamu jinsi gani wanahamasishwa kudai risiti za kieletroki pamoja na kufahamu elimu nzima ya kodi.
Afisa huyo aliyaeleza hayo, wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi, huko katika banda la Mamlaka hiyo kwenye maonesho ya siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete.
Alisema jambo kubwa ambalo wamelisongeza zaidi katika maonesho hayo, ni uwepo wa mfumo wa kukusanyia kodi mtandaoni ZIDRAS (Zanzibar Integrated Domestic Revenue Administrative System), ambao unarahisisha na kuokoa muda na gharala ya kufuata ZAR Ofisini.
“Kwa sasa mfanya biashara yoyote na mtu ambaye anataka kulipa kodi yake, sio lazima kwenda ofisini unaweza kwenda chamanangwe na ukasajiliwa kwenye mfumo huo, utaweza kulipa na kurudisha marejesho ya ZRA ukiwa sehemu yoyote ile na risiti yao ukapata,”alisema afisa huyo.
Alisema sasa hivi dunia na mitandao imekua, uwepo wa mfumo huo utaweza kuwa rafiki kwa wafanya biashara, katika kulipa na kufanya marejesho ya ZRA bila ya kwenda kwenye ofisi za mikoa au Ofisi kuu.
Akizungumzia lengo la kuwepo kwenye maonesho hayo, alisema ZRA huendeleza kusambaza uwelewa kwa jamii juu ya elimu ya kodi , kwa sababu jamii inaonekana iko nyumanyuma katika suala la elimu kwenye kodi.
“Tunapofanya hivi wateja wetu wanahamasika kwa wingi kulipa kodi, wapo watu wengi wanataka kulipa kodi ila wanashindwa kujua taratibu za kufuata,”alisema.
Aidha afisa Tehama huyo, alisema lengo jengine ni kusogeza huduma karibu na jamii kutokana na zohali nyingi walizonazo, ila kwenye maonesho ni rahisi kufika na kupata elimu huyo na mwisho kufanya maamuzi sahihi.
“Wanaotembelea maonesho haya wanaona jinsi gani huduma zetu zinavyotolewa, hapa tunatoa leseni, tunasajili biashara, tunasajili mashine hapa hapa na elimu ya kodi mtu anapatiwa,”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi kujenge tabia ya kudai risiti, kila wanapofanya matumizi na kuhakikisha wanaweka namba zao za simu ili kuweza kuingia katika kampeni ya SOMBA ZAWADI NA ZRA.
Nao baadhi ya wafanyabiashara na wananchi wameishukuru ZRA kwa kuwasogezea huduma kwenye maonesho hayo, kwani baadhi yao wanaona usumbufu kwenda Ofisi kuu kufuata huduma.
Ali Khamis Kombo mkaazi wa Madenjani, amesema uwepo wa maonyesho hayo yamewasaidia kupata huduma zao mbali mbali, ikiwemo kubadilisha leseni yake ya chombo cha moto.
Hata hivyo aliwataka wananchi wenzake wanaotembelea maonesho hayo, wasisahau kufika katika banda la ZRA kwa kupatiwa elimu mbali mbali ya kodi.
MWISHO