Friday, December 27

MAKALA MAALUM: MWANAMKE ALIEACHA ALAMA ZA MAENDELEO ZINAZOWASAIDIA WANANCHI.

NA AMINA AHMED MOH’D PEMBA.

KATIKA maisha watu huacha kumbukumbu ambazo wakiwa hawapo katika ajira au wamehamia eneo jengine hukumbukwa kwa vile huacha alama za maendeleo zisiofutika.

Kwa watu  wa jimbo la Chonga na vitongoji vyake ikiwemo Pujini na kwengineko kisiwani Pemba, mchango wa maendeleo katika maeneo yao  uliotolewa na aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa wa jimbo hilo kutoka mwaka 1985 hadi 1990 , Bibi Lela  Nassor Khamis, hautasahaulika.

Mbunge huyu mstaafu, ambaye umri wake sasa ni miaka 71,  hivi sasa anakaa Chanjaani, mjini Chake Chake,bado harakati zake za kukiletea maendeleo kisiwa cha Pemba huzungumzwa kwa kutolewa mfano bora wa kiongozi mwanamke katika jamii.

Wakati alipokuwa mbunge wa Chonga Bi Lela alizikuta changamoto nyingi zikiwakabili wananchi wa jimbo hilo na kupunguza kasi za kujipatia maendeleo ya kijamii na upatikanaji wa huduma mbali mbali.

Miongoni mwao ni kufuata mbali huduma za afya kwa vile kwa baadhi yao kituo kidogo cha afya cha jimbo hilo kilikuwa mbali na walipokuwepo.

Lakini kubwa zaidi, watu waliohitaji huduma za uchunguzi wa kitaalamu wa afya au kulazwa kwa matibabu iliwabidi wafunge safari hadi katika Hospitali ya Chake Chake.

Hapa  ikumbukwe wakati ule, karibu miaka 40 iliopita ,walitembea  masafa marefu, hali ya usafiri haikuwa nzuri kisiwani Pemba, Kwanza njia ilikuwa sio nzuri na vyombo vya usafiri vilikuwa vichache.

Sambamba na hilo pia wanavijiji hivyo walikuwa  wanakabiliwa na shida ya  maji safi na salama.

Mwandishi wa habari hizi  alipomtembelea mbunge huyu mstaafu nyumbani kwake Chanjaani  amesema baada ya kuwa Mbunge wa Chonga alichangisha fedha kwa ujenzi wa kituo cha afya

 “Kila mtu katika kijiji alitakiwa atoe alichokuwa nacho, mwenye mia tano, elfu moja au zaidi ili tujenge kituo bora cha afya jimboni’’Alieleza

Pamoja na juhudi hiyo aliyoichukua baadhi ya watu walikuwa wakmkebehi na kusema walishindwa wanaume kujenga kituo kikubwa cha afya angeweza yeye mwanamke.

Hata hivyo, kauli hizo hazikumvunja moyo na aliendelea na zoezi ili kusaidia watu wa jimbo lake ili kuondoa shida za matibabu.

” Kwa kushirikiana na wananchi tulichagua kamati  ya kusimamia  fedha za makusanyo na ujenzi na nilimchagua marehemu Bwana Abdalla Said awe msimamizi wa ujenzi kwa vile shughuli zake zilikuwa ni ujenzi wa majumba’’” Alisema  .

” Nilipokwenda Dodoma kwa vikao vya Bunge walikuwepo watu waliosimamia michango baada  ya muda mfupi ujenzi wa kituo cha Afya cha Dodo Pujini ulianza’’, alisema.

Juhudi zao ziliungwa mkono na aliyekuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, marehemu Dk Omar Ali Juma, kwa kutoa mifuko 100 ya saruji.

Alisema ujenzi ulifanywa kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wanafunzi kwa kuchota maji na kupiga matofali, baadaye walijenga kituo cha fya Kilindi, sambamba na kile kituo cha Chonga.

Bi Lela alisema alitamani kujenga nyumba za madaktari katika maeneo hayo, lakini bahati haikuwa upande wake kwa vile  awamu iliofuata ya Bunge nafasi  hilo ilishikwa na mtu mwengine .

” Niligombea na nikakosa  kwa kuwa kila mtu anayo aina yake ya uongozi, yule aliepata hakuendeleza nilipoacha na hapo tena kamati nilizounda  zikasambaratika kwa vile mikakati ya huyo kiongozi mwengine ilikuwa tafauti na yangu”, aliongeza.

WANAWAKE KATIKA KUWANIA  UBUNGE ZANZIBAR

Safari ya wanawake ya kushika nafasi ya ubunge majimboni  bado ni ngumu, katika uchaguzi wa mwaka 2020 walijitokeza wanaume 257 na kati yao 46 walishinda.

Wanawake waliojitokeza kuwa wagombea ni 81 na wanne  tu ndio waliofanikiwa kuingia Bungeni.

Katika kipindi  cha uchaguzi wa mwaka 2015 idadi ya wanawake walioshika uongozi katika Bunge kupitia majimbo  viti maalum na uteuzi wa Rais ilikuwa ni 126, sawa na asilimia 32  ya wabunge wote 393.

Takwimu zinaonyesha katika uchaguzi wa mwaka  1995  ni wanawake wanane  tu ndio  walijitosa kuwania ubunge majimboni huku 37 wakipata  nafasi hiyo kupitia viti maalum.

Idadi hiyo ilifikisha wanawake kuwa 45  sawa na asilimia 16 tu kwa vile Wabunge waliochagulia walikuwa 269.

Idadi iliongezeka  na kufikia asilimia 36 mwaka 2010 lakini haikuendelea na ilishuka  hadi asilimia 32 mwaka 2015.

Bi Lela alisema kupata kwake kuwa Mbunge ilikuwa kama bahati tu, hasa kwa vile hakuwa na elimu ya juu.

Alisema  alipokuwa mdogo hakusoma, bali alianza kusoma baada ya kuolewa na  kupata watoto wawili mume wake ambaye alikuwa mwalimu ndiye aliyemshauri ajiunge na madarasa ya elimu watu wazima (siku hizi inaitwa elimu mbadala).

Alisoma  kuanzia mwaka 1973, hadi kufika farasa la 11  lakini hakufanya vizuri katika mtihani wa darasa hilo katika Skuli ya Forodhani, mjini Unguja.

Hapo tena akachukua masomo kwa njia ya posta na kupata cheti cha  darasa la 12 na safri yake ya kujipatia elimu ikaishia hapo.

Mmoja wa majirani zake katika kijiji cha  Kilima Hodi ambacho kipo karibu na kijiji cha Pujini, Bi Fatma khamis alisema alikutana na Bi Lela  wakiwa  katika harakati za kisiasa Bi Lela akiwa na chama  cha CCM na yeye akiwa mwanachama wa CUF.

Lakini licha ya uhasama wa kisiasa uliokuwepo hawakufarakana na wamekuwa wakishauriana kwa mambo mbali mbali, ikiwa ni  pamoja na masuala ya siasa.

Bi Fatma alisema watu wa kijijini kwake na pujini walikuwa wanatafuta huduma za matibabu Chake kabla ya kujengwa kituo cha Afya kijijini kwao.

kwa upande wake Mussa Talib mkaazi wa Pujini amesema muanzilishi wa kituo hicho cha afya cha Pujini hamjui, lakini ukweli ni kwamba kuwepo kwake kumepunguza shida za kufuata huduma hio Chake Chake.

HISTORIA YAKE KATIKA UONGOZI IPOJE

Kuanzia mwaka 1983 Bi Lela aliteuliwa kushika nafasi ya katibu msaidizi mkuu wa Wilaya ya Chake Chake  wa Umoja wa Vijana wa CCM na kushika nafasi hiyo kwa miaka tisa.

Baada ya kupata  ushawishi kutoka kwa viongozi wa chama chake alijitosa kugombea  kupitia majimboni kupiga kampeni za kuomba kura za ubunge na kushika nafasi hiyo  jimbo la Chonga  1985.

Bi Lela  pia alikuwa Mbunge  wa viti maalum kupitia jumuia ya vijana wa Mkoa kusini Pemba , mjumbe wa baraza kuu taifa Tanzania, mjumbe Halmashauri kuu ya taifa (NEC) ya CCM, mjumbe baraza kuu la vijana kwa awamu tofauti .

Hivi sasa anakitumikia chama chake kama mmoja wa wazee wa CCM na mshauri katika kutatua changamoto za  jamii iliyomzunguka  .

Bi Lela alisema anafurahia kwamba ametembelea mikoa yote Tanzania na kujifunza mambo mengi mazuri  ambayo yalizidi kuimarisha utendaji katika uongozi wake .

Hata hivyo alisema mfumo wa vyama vingi  uliingia wakati alishakuwemo katika siasa hakutishika na  joto la kisiasa lililokuwepo wakati ule na alijiamini kujitosa kupambana na wanaume kugombea uongozi.

Kwa wakati ule na hadi sasa kwa kiasi fulani haukuwa uamuzi mwepesi kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hivyo aliwataka wanawake   wenzake wa rika zote  wasiogope chochote kwani hakuna kigumu sana katika kuongoza.

“Lililo muhimu ni kuzijua sheria na kanuni za uongozi ni hizi na siku zote kufanya jambo kwa maslahi ya unaowaongoza bila ya upendeleo au ubaguzi wa aina yeyote ile ndio uongozi ” .

Aliwataka vijana wa kike waende kugombea kwenye majimbo na kuwa tayari kushindana na wanaume ili watetee haki zao na kuyapatia ufumbuzi matatizo yao.

“Changamoto ni za kawaida, lakini endapo utajiamini na kujua unachotakiwa kufanya kama kiongozi hutotishika huko hakuna anaebakwa wala kuombwa rushwa ya ngono kama hatokuwa tayari kufanya hivyo” alifafanua.

Aliwataka akina mama na akina dada kuamka na waache kudharauliana, lakini washikamane na wanaume kwenda pamoja .

“Ni muhimu pia kutopikiana majungu wanawake kwa wanawake tunawapa mwanya wanaume kutuburuza juu ya hili nikiwa  mama, bibi pia nasema kuwa  milango ipo wazi kwa wote ambao watakaohitaji ushauri  juu ya siasa na uongozi’’, aliongeza.

Vituo hivyo vyote  kwa sasa vimefanyiwa maboresho zaidi  ikiwa ni pamoja na kuongezwa ukubwa na serikali kutokana na kuongezeka mahitaji ya wananchi  ndani ya maeneo hayo

Harakati za kisiasa za bibi huyu, ujasiri wake na mchango wake mkubwa wa kuiletea jamii maendeleo ni kielelezo kizuri cha namna mwanamke anaweza kuiongoza jamii kwa amani na furaha katika kujipatia maendeleo.

Mwisho.