Sunday, December 29

Kuweni waadilifu munaposimamia mitihani

MARYAM SALUM  ,PEMBA

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa amewataka wakuu wa vituo, wasimamizi na kamati za mitihani za mikoa na wilaya kufanya kazi zao kwa umakini na uadilifu kwa kuzingatia kanuni na miongozo ya baraza la mitihani la Zanzibar.

Alisema katika ufanyaji kazi huo pia  wakizingatia usalama wa vituo, ili kuzuwia udanganyifu na kulinda haki za watahiniwa wenye mahitaji maalum.

Kauli hiyo aliitowa huko Wizara ya Elimu Pemba wakati akitowa taarifa maalum kwa waandishi wa habari  kuhusu mitihani ya Taifa ya darasa la nne,saba na kidato cha pili kwa mwaka 2023.

Alieleza miongoni mwa haki ambazo wanatakiwa kuzizingatia ni pamoja na kuhakikisha kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalum wanaongezewa muda wa nusu saa kwa kila saa moja ya mtihani.

Alisema kwa wale ambao wana  uoni hafifu kuhakikisha wanapewa mitihani inayowahusu ya maandishi yaliyokuzwa na wenye mahitaji mengine wanapewa mitihani inayowahusu kulingana na mahitaji yao.

Alifahamisha mitihani ya Taifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa darasa la saba inatarajiwa kufanyika kuanzia Octoba 30 hadi Novemba 02 mwaka 2023, kwa upande wa darasa la nne itafanyika Novemba 06 hadi Novemba 08 mwaka 2023 ambapo kwa upande wa kidato cha pili  itafanyika Disemba 04 hadi Disemba 12 mwaka 2023.

Alisema “ jumla ya vituo vilivyosajiliwa kufanya mitihani mwaka huu 2023 ni 545 kwa darasa la nne, 451 kwa darasa la saba na 313 kwa kidato cha pili Unguja na Pemba”, alisema.

Alisema katika mtihani wa darasa la nne  Waziri Lela alisema jumla ya watahiniwa 58,485 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo na kati ya watahiniwa hao wanaume ni 29,832 sawa na asilimia 51 na wanawake 28,653 sawa na asilimia 49.

Aliendelea kusema kuwa katika mtihani wa darasa la saba jumla ya watahiniwa  44,684 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo na kati ya watahiniwa hao wanaume ni 21,430 sawa na asilimia 48, ambapo wanawake ni 23,254 sawa na asilimia 52.

Kwa upande wa mitihani ya kidato cha pili jumla ya watahiniwa 24,382 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo na kati ya watahiniwa hao wanaume ni 10,558 sawa na asilimia 43.3 na wanawake 13,824 sawa na asilimia 56.7.

“ Jumla ya watahiniwa 655 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo ,kwa upande wa darasa la nne ni 289 darasa la saba ni 242 na kidato cha pili ni 124”, alisema.

Alifahamisha kuwa maandalizi ya mitihani yamekamilika kwa kuhakikisha kuwa mitihani yote imeandaliwa vyema ,kuchapwa na kusafirishwa  katika ngazi za mikoa na wilaya na iko tayari kwa kufanyika.

Alisema wizara ya elimu ina matumaini makubwa  na watahiniwa  kuwa wamejiandaa vyema kukabiliana na mitihani hiyo kwa mujibu wa walivofundishwa na walimu wao.

Aidha aliwasihi watahiniwa wote kuzingatia kanuni za mitihani  na kutoshiriki katika udanganyifu wa aina yoyote na kuwasisitiza walimu wakuu kutowa ushirikiano unaotakiwa kwa wakuu wa vituo na wasiingilie vituo vya mitihani ama kusababisha udanganyifu.

“Nitowe wito tu kwa jamii kutowa ushirikiano unaotakiwa na kuhakikisha mitihani yetu ya mwaka huu inafanyika kwa amani na utulivu”, alisema.

Alisema moja ya jukumu kubwa kwa jamii ni kujiepusha na kupita pita katika maeneo ambayo mitihani inafanyika  na kwa kufanya hivyo itawasaidia watahiniwa hao kufanya mitihani kwa utulivu na amani.

Nae kwa upande wake Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Pemba , Mohamed Nassor Salim aliwataka wanafunzi na Walimu waliopewa jukumu la kusimamia mitihani hiyo kwa uadilifu mkubwa ili kuepusha kufutiwa matokeo yao.

Alisema ni vyema wasimamizi kutowaruhusu Wanafunzi kutoka toka ovyo kwenye chumba cha mitihani kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta picha mbaya kwao.

Hata hivyo aliwasihi Wananchi kuacha kujipitisha katika maeneo ambayo wanafunzi wanaendelea na mitihani yao ili kuwapa utulivu zaidi wa kujibu masuala walioulizwa katika Karatasi za Mitihani.

MWISHO.