MARYAM SALUM,PEMBA
WANANCHI wa Kijiji cha Mgogoni Chake Chake wamewataka wasaidizi wa haki za binaadamu Kisiwani Pemba kuendelea kutoa huduma ya elimu juu ya upatikanaji wa haki za kibinaadamu ili kuepusha migogoro inayoweza kuepukika.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huko kijijini kwao baada ya kumaliza mkutano wa utoaji elimu ya haki za binadamu kutoka kwa wasaidizi wa sheria jimbo la Wawi, wananchi hao walisema kuwa suala la elimu juu ya upatikanaji wa haki za kibinaadamu hasa vijijini ni jambo ambalo limekuwa likileta changamoto zaidi ndani ya jamii.
Maryam Juma Salum mkaazi wa kijiji hicho alieleza kuwa kumekuwa na migogoro mingi itokanayo na kesi mbali mbali ikiwemo masuala ya ndoa,malezi, ardhi, na mengine yanayofanana na hayo katika jamii,lakini hakuna mtu mwenye uelewa wa nani amtafute kwa ajili ya kupata msaada wa kisheria kabla yakufikishana mbali.
“Jamii inajua kwamba kila kosa linapatiwa ufumbuzi mahakamani tu na si pengine popote,kumbe ni tofauti na dhana hiyo, hivyo sasa baada ya elimu hii ya haki za binaadamu tumeshapata uwelewa wakutosha kwanza kuzifahamu haki za kibinaadamu na njia gani tunaweza kuzitumia pale inapotokezea matatizo madogo madogo kwa msaada,” alisema mwananchi huyo.
Juma Issa Juma mkaazi wa shehia ya Mgogoni alisema kuwa kijiji cha mgogoni ni kijiji ambacho kinamatatizo mengi hasa ya wizi, lakini inapotokezea kijana amefanya kosa la wizi, au ugomvi basi familia hukimbilia Polisi moja kwa moja ili kupata msaada na kupatiwa suluhu ya tatizo.
“Hivyo baada ya elimu hii tuliyopatiwa na wasaidizi wa sheria katika upatikanaji wa haki za kibinaadamu tunaimani jamii ya mgogoni imefumbuka vyakutosha na watakuwa wajumbe kwa wengine ambao hawakusikia elimu hii na pale ikitokezea labda kesi hasa zile ndogo ndogo tusikimbilie Polisi moja kwa moja kwani wapo wasaidizi wa sheria wataweza kutatua changamoto kwa njia moja ama nyengine kwa mujibu wa sheria,” aliofahamishwa.
Aidha aliahidi kwamba elimu waliyopewa juu ya upatikanaji wa haki za vinaadamu, kama jamii wataifanyia kazi ili ikitokezea makosa hasa madogo madogo watashirikiana nao kuona inaipunguzia Serikali mzogo mzito wa mkondomano wa kesi mahakamani ambazo hata wao wanaweza kusuluhisha na tatizo likaondoka bila ya mtu kufikishwa kwenye vyombo vikuu.
Mapema msaidizi wa sheria kutoka Jimbo la Wawi Haji Nassor Mohamed akitoa elimu kwa wananchi hao juu ya upatikanaji wa haki za binaadamu alisema kuwa kazi kubwa ya wasaidizi wa sheria ni kukutana na wananchi kuona wanawafahamisha watu haki za kibainaadamu ni zipi na jinsi ya kuzipata.
Alisema kuwa wasaidizi wa kisheria katika upatikana wa haki za kibinadamu wapo kila shehia na lengo lake ni kusaidia wananchi katika kuwapatia msaada wa kisheria juu ya tatizo mtu ambalo limemkuta.
“Sisi kazi yetu kubwa ni kuelimisha jamii juu ya haki za binadamu ni zipi, na pale ikitokea changamoto kwa hatua ya mwanzo kabla ya kwenda polisi moja kwa moja kwanza aweze kupata msaada wa kisheria wapi kwani inawezekana tatizo ambalo analo halihitaji kufika huko,” alisema.
Alieleleza kuwa haki za kibinaadamu ni zile haki alizonazo mtu baada ya kuzaliwa ama kwa ubinaadamu wake.
Alifahamisha kuwa haki kibinaadamu zipo nyingi , ingawa jamii wanaelewa ile ya kupiga kura,afya,elimu, lakini hata malazi bora, makuzi bora, kushirikishwa,kujikusanya pamoja kwa ajili ya shuhuli za maendeleo, na utoaji maoni na kupata taarifa na nyengine zilizofanans na hizo.
Aidha wasaidizi wa sheria wapo kujitolea zaidi, lengo ni kuhakikisha jamii inapata uwelewa wa kila jambi katika upatikanaji wa haki za kibinaadamu.
Sambamba na hayo aliwataka wananchi kuitumia elimu hiyo wanayowapatia wawatumie wasaidizi wa sheria katika shehia zao, ili kuondosha usumbufu.
Kwa upande wake sheha wa shehia hiyo Suleiman Nassor Suleiman alieleza kuwa katika shehia yake yapo matokeo mengi ambayo yanahitaji tu msaada wa kisheria kwa ajili ya suluhisho bila polisi walk mahakamani.
“Yapo matukio yakupelekana polisi hadi mahakamani, lakini si kesi kama ya ugomvi wa mara moja, watoto kwa watoto kupigana, uharibifu wa mazao kupitia mifugo, hasa ni masuala yanayohitaji msaada tu kutoka kwa wengine ili kupatiwa ufumbuzi,”. alisema sheha.
Hivyo aliwataka wananchi na jamii kwa ujumla kyona kwamba elimu hiyo inahitaji kufanyiwa kazi ili ifike pahala polisi na mahakamani zinabaki zile kesi kubwa kama ubakaji, unyanyasaji,na mengine makubwa zaidi yaliyofanana na hayo, kwani lengo la kiwepo kwa hawa wasaidizi wa sheria katika upatikanaji wa haki za kibinaadamu nikuisaidia Serikali kuiondoshea mzigo mzito.
MWISHO.