Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewapongeza Waumini pamoja na Wananchi Nchini kwa utulivu wao mkubwa unaotoa faraja kwa Serikali Kuu kuendelea kujipanga katika kukabiliana na matatizo na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wakati akitoa salamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kijiji cha Mwache Alale Jimbo la Mfenesini Wilaya ya Magharibi A Mh. Hemed alisema nguvu za pamoja zinahitajika ambazo ndio msingi pekee wa kuelekea kwenye mafanikio ya maendeleo yatakayonufaisha Serikali na Wananchi wake.
Akitoa Shukrani Mwakilishi wa Waumini na Wananchi wa Kijiji cha Mwache Alale Mzee Ameir amemthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wao wako pamoja na maamuzi yanayochukuliwa na Viongozi wao mambo ambayo waliyatarajia kutokana na kasi ya uwajibikaji wa Serikali.
Mwakilishi wa Waumini na Wananchi hao wa Kijiji cha Mwache Alale ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia changamoto zinazowakabili Wananchi hao za ubovu wa Bara bara iendayo Kijiji hicho inayoviza maendeleo yao hasa huduma za Kielimu kutokana na Walimu kuchelewa madarasani.
Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)