Wednesday, January 1

Dk. Mwinyi ataka usafi kwenye miji uimarike

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amezitaka Halmashauri, Mabaraza ya Miji na Manispaa kudumisha usafi katika miji, ili kuweiweka katika mazingira bora na haiba ya kuvutia.
Akizungumza wakati akifungua kituo cha wajasiriamali Kifumbikai Wete pamoja na stendi ya Kinowe Konde Dk. Mwinyi aliziagiza taasisi hizo mambo matano, ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika miji, kujenga masoko, vituo vya ujasiriamali, maegesho na viwanja vya kufurahishia watoto ambayo hayo yatasaidia kuweka mazingira bora na mazuri.
Alisema kuwa, usafi ni muhimu katika maisha ya mwanadamu, hivyo ni wajibu wao kudumisha katika maeneo ya miji, kwa ajili ya kuweka mandhari nzuri na ya kuvutia.
“Tumebadilisha ugatuzi ili taasisi hizi ziweze kufanya kazi zake vizuri ikiwa ni pamoja na suala la kuimarisha usafi katika miji yetu, hivyo mna wajibu wa kuyatekeleza kwa vitendo ili kuimarisha maisha ya wananchi,” alisema Rais Mwinyi.
Aidha Dk. Mwinyi alieleza kuwa, kituo hicho cha wajasiriamali pamoja na stendi (maegesho) alizozifungua ni fursa muhimu ya kiuchumi kwa wananchi ambayo watafanya biashara katika maeneo hayo na kujipatia fedha zitakazowakwamua na maisha duni.
“Wakati nafanya kampeni wajasiriamali walitaka wapatiwe mtaji, maeneo mazuri ya kufanya biashara zao na kodi nafuu, ambapo kwa miaka mitatu ya awamu ya nane tayari imeshatekeleza hayo kwa kiasi kikubwa, kwani jumla ya shilingi bilioni 31 zimetengwa kwa ajili ya kuwapatia mikopo wajasiriamali bila ya riba kupitia benki ya CRDB,” alifafanua.
 Dk. Mwinyi aliagiza Mamlaka husika kutowatoza kodi miezi mitatu kwa wajasiriamali ambao watakwenda kuuza bidhaa zao kwenye soko hilo, huku akisisitiza kupewa kipao mbele katika suala la kupatiwa mikopo, ili wajipatie mtaji utakaowasaidia katika shughuli zao za ujasiriamali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema kuwa, Dk. Mwinyi amefanya mambo makubwa ambayo yataimarisha maisha ya wananchi na kupata maendeleo.
“Tutayasimamia majengo haya na kudumisha usafi kwenye vituo, masoko na maeneo mengine ya miji ili wafaidike wao na vizazi vijavyo,” alieleza Mkuu huyo.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMS Massoud Ali Mohamed alisema kuwa, Dk. Mwinyi anatimiza ahadi zake kwa vitendo ambapo kwa miaka mitatu ya uongozi wake ameshajenga vitu 25 kwa wilaya 11 za Zanzibar.
“Lengo la Rais kujenga vituo hivyo ni kuwainua wananchi kiuchumi ili wawe na kipato kizuri kitakachowakwamua kimaisha na kupata maendeleo endelevu, hivyo mengi yamefanyika katika sekta mbali mbali na yanaendelea kufanyika,” alifafanua Waziri huyo.
Mapema Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya walisema, wamepata faraja kuzinduliwa kituo cha wajasiriamali na stendi kwani vitaimarisha maisha ya wananchi kiuchumi.
Mapema wafanyabiashara wa kituo cha wajasiriamali Kifumbikai Wete walisema kuwa wamefurahi sana kwani watajikwamua kimaisha na kuiomba Serikali iwapunguzie kodi ili wanufaike zaidi.
Ujenzi wa kituo cha wajasiriamali kimegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5 huku stendi ya Kinowe Konde ikigharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.4.
                       MWISHO.
*****************”””””””””””””“”****””””””””””””””**********
Serikali itaendelea kujenga hospitali, kuifarakisha huduma za afya

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kujenga hospitali na vituo vya afya vyenye vifaa vya kisasa ili kuwapatia huduma bora za afya wananchi wake.
Akizungumza wakati akifungua hospitali ya Wilaya iliyopo Kinyasini Wilaya ya Wete, Dk. Mwinyi alisema tayari zimeshajengwa hospitali  za Wilaya kwa unguja na Pemba huku Serikali ikiendelea kujenga hospitali za mikoa, rufaa na mwanzo (dispensaries na vituo vya afya) ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila ya usumbufu.
Alisema kuwa, ujenzi wa hospitali hizo na vituo vya afya vitawapunguzia wananchi kwenda masafa marefu kuifuata huduma hiyo, sambamba ya kupata huduma bora kutokana na vifaa vya kisasa vilivyowekwa.
“Tutahakikisha tunasogeza huduma bora za afya kwa wananchi, ili wawe na afya njema na sehemu ambazo bado hatujajenga basi wananchi wawe na imani kwani Serikali itawajengea ambapo kuna mradi wa shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali na vituo vya afya,” alieleza Dk. Mwinyi.
Aidha Dk. Mwinyi aliitaka Wizara waongeze wafanyakazi pale ambapo kunahitajika, kuwalipa watoa huduma na kuhakikisha maslahi yao yatapatikana kwa wakati ili wafanye kazi ya kutoa huduma kwa bidii.
“Majengo bila huduma sio kitu, hivyo endeleeni kutoa huduma bora kwani vifaa vya kisasa vipo kwa hiyo hakuna sababu ya kutokutoa huduma bora kwa sababu maslahi yenu tunayazingatia ,” alieleza Rais huyo.
Dk. Mwinyi aliwataka madaktari kufanya kazi kwa bidii na kujifunza mbinu mpya kutoka kwa wataalamu wanaofika katika hospitali hizo, ili wawe na uwezo mzuri wa kutoa huduma.
Pia aliwataka kuwa na moyo wa kujitolea katika kufanya kazi zao huku wakiacha ukali na lugha chafu wakati wa kuwahudumia wagonjwa kwani lugha chafu ni sababu ya kumuongezea mgonjwa maradhi.
“Majengo haya muyasimamie na kutunza vifaa vilivyomo ili vitumike kwa muda mrefu na wananchi wapate kunufaika,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazuri alisema kuwa, zaidi ya shilingi bilioni 7 zilitumika kwa ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na vifaa, ambapo ina uwezo wa kulazwa wagonjwa 100 kwa wakati mmoja.
“Miaka mitatu ya Dk. Mwinyi amefanya makubwa kwenye sekta ya afya, hivyo ni vyema tukazithamini juhudi hizi kwa kuendelea kuchapa kazi ili lengo la kutoa huduma bora za afya zifikiwe ipasavyo,” alieleza.
Nae Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, kwa sasa huduma za afya zimeimarika katika Mkoa wake na wananchi wanapata matibabu bora.
“Tunamshukuru Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaletea huduma bora za afya, anahitaji kupewa pongezi kutokana na mambo anayoyafanya,” alifahamisha.
Mwananchi Aisha Ali Massoud na Hassan Salim Bakar waliishikuru Serikali kuwajengea hospitali hiyo kwani wamepunguza masafa sambamba na kuimarisha uchumi wa vijiji vyao.
Walisema kuwa, wanatarajia kupata huduma mbali mbali za vipimo bila ya usumbufu wowote na kueleza kuwa wataendeleza ushirikiano kama ambavyo walishirikiana na wajenzi wa hospitali hiyo.
                 MWISHO.