NA AMINA AHMED-PEMBA.
Waalimu Kisiwani Pemba wametakiwa kuzitumia fursa za kujiunga na Mifuko ya bima ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maisha ikiwemo, Afya mali, Ajali pamoja na majanga mengine mbali mbali.
Ushauri huo umetolewa na mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali alipokuwa akizungumza na waalimu katika ufunguzi wa mafunzo maalumu ya utowaji wa elimu ya bima yalioandaliwa na mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA kwa wanachama wa Saccos ya walimu Pemba yaliofanyika katika ukumbi wa Tibirinzi Chake Chake Pemba .
Amesema kujiunga na Bima mbali mbali ni moja kati ya hakiba zitakazosaidia kukabiliana na majanga yasioepukika kwa mtu mmoja mmoja au kikundi na kuweza kupata usaidizi wa kujikimu pindi yanapotokea.
Aidha Rashid Ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoendelea kulalamikiwa na wanachama wanaojiunga na bima mbali mbali ikiwemo kucheleweshewa fidia wanapopatwa na majanga pamoja na kuchelewa kupatiwa bima mpya kwa baadhi ya bima ambazo zimemaliza muda wake.
Naibu kamishna wa Mamlaka hiyo Zanzibar Khadija Issa Said amewataka walimu hao kisiwani Pemba kuanzisha uwakala wa bima katika Taasisi zao Ili kurahisisha kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo kwa urahisi.
Amesema mamlaka hiyo inayotambulika kisheria itaendelea kuratibu na kusimamia shughuli za bima bara na visiwani Zanzbar kwa lengo la kusajili na kusimamia huduma za bima nchini, kutoka kwa kampuni, mashirika na taasisi ili kuona malengo ya kuanzishwa kwa sekta hizo yanaendelea kufikiwa na kuwanufaisha wanachama wake.
Akitoa neno la shukuran kwa niaba ya Walimu kutoka Saccos ya walimu Pemba Said Suleiman ameishukuru taasisi hiyo kwa kuwapa elimu juu ya bima mbali ambazo zitasaidia kutatua changamoto zinazojitokeza kila siku katika maisha.
Utolewaji wa elimu ya bima kwa Saccos ya walimu Pemba yameandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Bima ya Jubilee Life Insurance imewashirikisha zaidi ya waalimu 150 ambapo jumla ya mada 3 zimewasilishwa ikiwemo Bima ya maisha kwa na vikundi, bima ya elimu, pamoja na bima ya afya.
mwisho .