Saturday, December 28

SMZ itaendelea kuipa kipaombele Sekta ya Michezo hasa michezo Jumuishi.

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuipa kipaombele Sekta ya Michezo hasa michezo Jumuishi ili kutoa fursa kwa watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu kujumuika pamoja katika kujifunza na kushiriki katika michezo mbali mbali pasipo na utenganishi miongoni mwao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduziu Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo katika Hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akifungua Warsha ya Kimataifa kuhusu Skuli na Michezo Jumuishi katika Ukumbi wa Hotel Verde Mtoni jijini Zanzibar.

Amesema kuwepo na Michezo Jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kutasaidia kukuza na kuhuisha ushiriki wa watu wenye ulemavu hususan ulemavu wa akili kwenye mashindano mbali mbali ya michezo ndani na nje ya nchi.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali zote mbili kwa kutambua umuhimu wa michezo zimeamua kuipa kipaumbele sekta ya Michezo kwa kuhakikisha nchi inakuwa na Viwanja vyenye hadhi ya Kimataifa sambamba na kuboresha viwanja vya michezo katika skuli za Tanzania bara na Zanzibar.

Aidha Mhe. Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi amefahamisha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kujenga kiwanja kikubwa cha Michezo Jijini Dodoma kitakacho julikana kwa jina la Dodoma Sports Complex na kuviboresha vyengine saba ili kukuza sekta ya michezo.

Kwa upande wa Zanzibar Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuufanyia ukarabati mkubwa Uwanja wa Amani kwa Unguja na ule wa Gombani Pemba kwa lengo la kukuza sekta ya michezo nchi sambamba na kujenga kiwanja cha Micheao cha kisasa kilichopo Matumbaku Wilaya ya Mjini kinachojumuisha viwanja vinne ndani yake sambamba na kujenga viwanja vya Michezo katika Wilaya zote kumi na moja (11) za Zanzibar .

Amesema kwa kutambua umuhimu wa michezo Serikali zote mbili zimewapa fursa watu wenye ulemavu na kuwawezesha kushiriki katika mashindano ya Kimataifa yanayofanyika nchi mbali mbali Duniani na kusema kuwa serikali zitaendelea kusimamia na kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa ya kujitangaza ndani na nje ya nchi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema mafunzo hayo ya Skuli na Michezo Jumuishi yatakuwa chachu ya kupata wataalamu wa kuwafundisha watu wenye ulemavu wa akili waliopo maskulini na maeneo mengine ya nchi zetu ili kuweza kushiriki kikamilifu katika Michezo Jumuishi.

Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita amesema Wizara ya habari itaendelea kutoa mashirikiano katika kuhakikisha kuwa Michezo Jumuishi inapewa kipaombele hapa nchini ili kutoa nafasi kwa watu wenye ulemavu wa akili kushiriki katika michezo ndani na nje ya nchi.

Amesema kuwa wanamichezo walemavu wamekuwa wakifanya vizuri katika michezo mbali mbali ambayo wanashiriki na kuipatia heshima kubwa nchi yetu.

Waziri Tabia ameiomba Serikali kuangalia kwa ukaribu uwezekano wa kuongeza Bajeti katika fungu la Michezo kwa mwaka wa fedha ujao ili kutoa nafasi kwa watu wenye ulemavu kuweza kushiriki katika michezo mbali mbali sambamba na kuomba kuangaliwa kushiriki katika Sherehe za Mapinduzi.

Kwa upande wake Raisi wa michezo ya Olimpic Afrika CHARLES NYAMBE amesema kushiriki katika michezo ya olimpic kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo yenye ulemavu waakili kumewasaidia wanafunzi hao kukuwa kiakili na kimaarifa jambo ambalo linatoa matokeo chanya katika mashindano wanayoshiriki.

Amesema kushiriki kwa wanafuzi katika michezo Jumuishi kwenye maskuli kunawafanya wanafunzi wenye mahitaji maalum na wenye vipaji kuweza kujitangaza na kujiajiri kupitia vipaji vyao katika michezo.

Jumla ya Nchi kumi na tatu Brani Afrika zinashiriki katika mafunzo hayo ambapo kwa mwaka huu 2023 Zanzibar ndio mwenyeji wa Mafunzo hayo.

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)
Leo tarehe 13.11.2023